Watoto wawili wafariki baada ya moto kuzuka nyumbani kwao Kirinyaga

Watoto wawili wamefariki wakati wa kisa hicho, lakini watu kadhaa waliachwa bila makao

Muhtasari

•Watoto wawili wamefariki wakati wa kisa hicho, lakini watu kadhaa waliachwa bila makao.

•Wakazi wa Kagumo na wazima moto kutoka Serikali ya Kaunti ya Kirinyaga walipata shida kuzima moto huo.

Picha ya nyumba inayowaka moto
Image: Hisani

Watoto Wawili Wafariki Baada ya Moto Kuzuka Nyumbani Kwao Kirinyaga

Polisi katika Kaunti ya Kirinyaga wanachunguza kisa cha moto ulioua watoto wawili katika Kituo cha Biashara cha Kagumo eneo bunge la Kirinyaga ya Kati Jumatatu usiku.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa nane mchana, ambapo watoto wawili wenye umri wa miezi 4 na miaka 4 waliteketea kiasi cha kutotambulika.

Kulingana na polisi, mama wa watoto hao wawili alikuwa ameenda sokoni kununua chakula cha jioni wakati kisa hicho kilipotokea.

Wakazi wa Kagumo na wazima moto kutoka Serikali ya Kaunti ya Kirinyaga walipata shida kuzima moto huo.

"Watoto wawili wamefariki wakati wa kisa hicho, lakini watu kadhaa waliachwa bila makao," Jane Wanjiku alisema.

MCA wa eneo hilo David Kinyua Wangui, ambaye alifika katika eneo la tukio mara moja, alisema zaidi ya nyumba 20 za mbao zilizokodiwa ziliharibiwa na kuwa majivu. "Tunaomba msaada kwani wamelala kwenye baridi," Kinyua alisema.

Kamishna wa Kaunti ya Kirinyaga Hussein Alasow alisema moto huo ulianza katika moja ya nyumba zilizoathiriwa kabla ya kuenea haraka hadi kwa nyumba zingine za mbao.

"Chanzo cha moto huo bado hakijabainika. Tumeanzisha uchunguzi," kamishna huyo wa kaunti alisema.

Miili miwili iliyoteketea kiasi cha kutotambulika ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Kerugoya.