Gavana Sakaja aondoa agizo la kusitisha vibali vya ujenzi

Muhtasari

•Sakaja alikuwa amesitisha uidhinishaji mpya wa mipango ya majengo na uchimbaji katika maeneo ya ujenzi wakati wa mvua kubwa iliyonyesha hivi majuzi na kusababisha mafuriko.

•Pia aliagiza kukaguliwa kwa maeneo ya ujenzi na majengo ambayo yaliidhinishwa kwa muda wa miezi 24 iliyopita ili kuhakikisha yanakidhi viwango.

Gavana Sakaja. Hisani:Instagram
Gavana Sakaja. Hisani:Instagram

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ameondoa agizo la kusitisha mchakato wa uidhinishaji wa mpango mpya wa majengo na uchimbaji katika maeneo ya ujenzi ndani ya jiji.

Sakaja aliweka marufuku hayo Aprili 29 katika kipindi cha mvua kubwa, pia aliagiza ukaguzi wa maeneo ya ujenzi na majengo ambayo yameidhinishwa kwa muda wa miezi 24 iliyopita ili kuhakikisha uzingatiaji wa kanuni zilizowekwa.

"Marufuku ya uchimbaji wa maeneo mapya ya ujenzi pia imeondolewa mara moja. Kusitishwa kwa mahitaji ya idhini na msamaha wa malipo ya ada ya ukarabati unaohusiana na mafuriko pia imeondolewa," Sakaja alisema katika taarifa yake kwa vyumba vya habari.

Aliongeza kuwa serikali ya Kaunti ya Nairobi tangu wakati huo imeanzisha mchakato wa kuunda jopo kazi la kukagua maeneo ya ujenzi ambayo yaliidhinishwa kwa muda wa miezi 24 iliyopita.

Kufuatia hili Serikali ya Kaunti ya Jiji la Nairobi (NCCG) kupitia afisi ya kaimu Katibu wa Kaunti imewaandikia washikadau mbalimbali ikiwaomba kuwasilisha majina ya wataalamu na wawakilishi ambao sasa watakuwa sehemu ya jopo kazi.

Jopo kazi itakutakana 12 Juni ili kuanza zoezi la ukaguzi katika jiji zima," alisema. 

Sakaja alisema kikosi hicho kina siku 60 za kukamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti kwa ofisi ya gavana kwa ajili ya utekelezaji.

Sakaja vile vile aliunda upya Kamati ya Ufundi ya Mjini (UPTC) kwa kutoa wito wa uwakilishi mpya kutoka kwa washikadau ambao ni pamoja na wasanifu majengo, wapangaji wa mipango miji, wanamazingira na wahandisi miongoni mwa wengine.