Mjane wa aliyekuwa mbunge wa Kibwezi Kalembe Ndile afariki

Hadi kifo chake, alikuwa MCA aliyeteuliwa na bunge la kaunti ya Makueni.

Muhtasari

•Magdalene Kalembe, MCA mteule katika Bunge la Kaunti ya Makueni chini ya Chama cha Maendeleo Chap chap, alifariki Jumanne usiku baada ya kuugua kwa muda mfupi.

•Kulingana na msemaji wa familia hiyo Sam Ndile, Magdalene aliugua siku ya Alhamisi na kulazwa hospitalini.

Magdalene Kalembe, MCA mteule katika Bunge la Kaunti ya Makueni chini ya Chama cha Maendeleo Chap chap
Image: VERONICA NTHAKYO

Mke wa aliyekuwa mbunge wa Kibwezi Kalembe Ndile amefariki dunia.

Magdalene Kalembe, MCA mteule katika Bunge la Kaunti ya Makueni chini ya Chama cha Maendeleo Chap chap, alifariki Jumanne usiku baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Kulingana na msemaji wa familia hiyo Sam Ndile, Magdalene aliugua siku ya Alhamisi na kulazwa hospitalini.

Alifariki alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya MP Shah jijini Nairobi.

"Magdalene aliugua Alhamisi akiwa katika Bunge la Kaunti na kusafiri hadi Nairobi ambako alilazwa, hali yake ilizidi kuwa mbaya Jumanne jioni. Alihamishiwa ICU ambako alituacha," alibainisha Ndile.

 Kiongozi wa Chama cha Maendeleo Chap Chap na Waziri wa Utalii Alfred Mutua akithibitisha habari hizo alisema Magdaline aliugua mwishoni mwa wiki jana na alikuwa akitibiwa homa ya dengue.

"Rambirambi zangu za dhati zinaenda kwa familia ya Kalembe/Nguluku, marafiki, na wote waliomfahamu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi," alisema.

Waziri huyo alisema matangazo zaidi yatafuata baada ya mashauriano na familia.

"Mola wetu ailaze roho yake amani ya milele," aliongeza.