KNCCI yaahirisha mkutano wa Kisumu, rais Ruto alitarajiwa kuhudhuria

Kongamano hilo la uwekezaji lilipaswa kufanywa kati ya Juni 28 na 29 huku rais William Ruto akiwa mgeni mkuu

Muhtasari

•Mwenyekiti wa kongamano la kimataifa la uwekezaji la Nyanza, Japh Olende alitangaza kuwa hafla hiyo inasitishwa kutokana na maandamano yaliyoshuhudiwa kote nchini.

•Ruto alipaswa kuwasili Kisumu mnamo Ijumaa, Juni 28, kufungua kongamano hilo la siku mbili.

Image: BBC

Chama cha wafanyabiashara na wenye viwanda nchini (KNCCI)  kilitangaza kuwa kinaghairi kongamano la uwekezaji ambalo lilipaswa kufanywa Kisumu.

Katika chapisho la siku ya Jumanne ,kupitia kwa mwenyekiti wa kongamano la kimataifa la uwekezaji la Nyanza, Japh Olende alitangaza kuwa hafla hiyo inasitishwa kutokana na maandamano yaliyoshuhudiwa kote nchini.

Kongamano hilo lilipaswa kufanywa kati ya Juni 28 na 29 huku rais William Ruto akiwa mgeni mkuu. Ruto alipaswa kuwasili Kisumu mnamo Ijumaa, Juni 28, kufungua kongamano hilo la siku mbili.

"Kwa kuzingatia hali iliyopo nchini, sisi, kamati ya maandalizi ya kongamano la kimataifa la uwekezaji la Nyanza, tumefikia uamuzi wa kuahirisha mkutano huo hadi tarehe nyingine," taarifa kutoka KNCCI ilisoma kwa sehemu.

"Tutakujulisha kuhusu tarehe mpya za mkutano baada ya mapitio ya kina ya vigezo muhimu vinavyohitajika ili kuhakikisha mkutano wenye mafanikio."

Hafla hiyo ilipaswa kuwaleta pamoja wawekezaji wa ndani na wa kimataifa pamoja na uongozi mkuu wa nchi kutafuta fursa za uwekezaji katika eneo la Nyanza.

Kisumu ilikuwa sehemu ya mikoa ambayo ilikumbwa na maandamano makubwa huku vijana kwa maelfu wakijitokeza barabarani kupinga mswada wa fedha wa 2024.