Rais Ruto kuhutubia taifa saa kumi jioni

Hii ni hotuba ya pili kwa Rais katika muda usiozidi saa 24 baada ya kulihutubia taifa baada ya maandamano siku ya Jumanne.

Muhtasari

•Kuligana na mwaliko uliotumwa kwa meza yetu ya habari, mkutano huo utafanyika Ikulu ya Nairobi.

Rais William Ruto
Rais William Ruto
Image: PCS

Rais William Ruto anatazamiwa kuhutubia taifa saa kumi jioni siku ya Jumatano.

Kuligana na mwaliko uliotumwa kwa meza yetu ya habari, mkutano huo utafanyika Ikulu ya Nairobi.

Hotuba ya Rais inajiri muda mfupi baada ya habari kuibuka kwamba rais alidida kutia saini mswada wa fedha 2024/25.

Vyanzo vya habari vya Ikulu viliiambia  meza yetu  ya habari kuwa Muswada huo utarejeshwa Bungeni kabla ya mapumziko leo.

Mkuu wa Nchi amependekeza rafu ya marekebisho ya Mswada huo.

Bunge linaweza kurekebisha Mswada huo kwa kuzingatia kutoridhishwa na rais au kuupitisha mara ya pili bila kuufanyia marekebisho.

Katika kurejesha mswada huo, rais ataonyesha maeneo muhimu ambayo yanahitaji kubadilishwa.

Iwapo wabunge watarekebisha mswada huo ili kuafiki kutoridhishwa kwa Rais kikamilifu, spika atauwasilisha tena kwa rais ili apate kibali.

Iwapo Bunge litazingatia kutoridhishwa kwa rais, linaweza kuipitisha mara ya pili, bila marekebisho, au kwa marekebisho ambayo hayatoshelezi kutoridhishwa kwake kikamilifu.

Hii lazima, hata hivyo, iwe imeungwa mkono na theluthi mbili ya wanachama.

Huku wabunge hao wakitarajiwa kwenda mapumzikoni kuanzia leo hadi Julai 23, ina maana kwamba iwapo Rais atarejesha mswada huo Bungeni huenda spika atalazimika kuwarejesha.

Baadhi ya mapendekezo ya kodi ambayo awali yaliletwa katika muswada huo ni pamoja na asilimia 16 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mkate, Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya mboga, VAT kwenye usafirishaji wa sukari, asilimia 2.5 ya Ushuru wa Magari na Ushuru wa mazingira kwa bidhaa zinazotengenezwa nchini.