UDA yaahirisha uchaguzi wa mashinani katika Kaunti 14

"Kwa sababu zisizoepukika, Bodi imeamua kuwa ni muhimu kuahirisha uchaguzi wa mashina "

Muhtasari

•UDA katika taarifa yao imebaini kuwa uchaguzi uliokuwa ufanyike Juni 28 na 29 umeahirishwa kwa muda usiojulikana.

•Wagombea waliombwa kusubiri mawasiliano zaidi kutoka kwa chama iwapo tarehe mpya itapangwa katika siku zijazo.

Katibu mkuu wa UDA Cleophas Malala
Katibu mkuu wa UDA Cleophas Malala
Image: Facebook

Muungano wa Kidemokrasia wa (UDA) Jumatano, ulitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi za mashinani katika kaunti 14.

UDA katika taarifa yao imebaini kuwa uchaguzi uliokuwa ufanyike Juni 28 na 29 umeahirishwa kwa muda usiojulikana.

Wagombea waliombwa kusubiri mawasiliano zaidi kutoka kwa chama iwapo tarehe mpya itapangwa katika siku zijazo.

Kaunti zilizoathiriwa ni pamoja na Mombasa, Uasin Gishu, Nyandarua, Tharaka Nithi na Machakos, Kisii, Bungoma, Siaya, Taita Taveta, Wajir, Kwale, Kitui na Garissa.

"Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya Muungano wa chama cha UDA inatoa notisi hii rasmi kuhusu uchaguzi wa mashina uliopangwa kufanyika tarehe 28 na 29 Juni, 2024," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

"Kwa sababu ya hali zisizoepukika, Bodi imeamua kuwa ni muhimu kuahirisha uchaguzi wa mashina uliotajwa hapo juu"

Uchaguzi huo uliahirishwa wakati ambapo taifa limekumbwa na maandamano makubwa kutokana na Mswada wa Fedha wa 2024 ulioondolewa sasa.

Wakenya wameonyesha kutoridhishwa kwao na chama tawala na kusababisha uharibifu wa mali inayohusishwa na wanasiasa wa UDA.

Chama cha UDA hakikuonyesha kama maandamano au kulengwa kwa viongozi wa UDA na waandamanaji kulifahamisha uamuzi wa kufuta uchaguzi wa mashinani.