Mahakama yaamuru polisi kutotumia vitoza machozi wakati wa maandamano

Polisi wameonywa dhidi ya kutumia risasi ,silaha ghafi na hatua nyingine katili za kuwatawanya waandamanaji

Muhtasari

•Saitabao Ole Kanchory aliwasilisha kesi katika mahakama kuu akitaka polisi kutotumia silaha ghafi wakati wa kuwatawanya waaandamanaji.

•Jaji Mugure Thande alitoa amri wakati wa kikao cha mahakama kuu kule Malindi,Juni 28 2024.

Image: CYRUS OMBATI

 Mahakama kuu imetoa agizo la kuzuia huduma ya polisi ya kitaifa kutumia nguvu kupita kiasi, ikiwa ni pamoja na maji ya kuwasha na mabomu ya machozi, dhidi ya waandamanaji wa amani.

Kwenye kesi iliyowasilishwa na Saitabao Ole Kanchory ambaye alikuwa baadhi ya vingozi wa Azimio,  Jaji Mugure Thande aliamuru maafisa wa polisi kutotumia risasi za moto, risasi za mpira, silaha ghafi na hatua nyingine za kikatili kuwatawanya waandamanaji.

Vilevile mahakama ilisisitiza kwamba polisi lazima wajizuie kutumia nguvu za kikatili, ghasia, au kufanya mauaji ya kiholela dhidi ya wale wanaotumia haki yao ya kukusanyika kwa amani.

Zaidi ya hayo, mahakama iliagiza watekelezaji sheria kukomesha kukamatwa kwa watu bila ya lazima, utekaji nyara, kuwekwa kizuizini, unyanyasaji, vitisho, utesaji, ukatili, unyama na udhalilishaji wa waandamanaji wanaoandamana kwa amani.

Katika ombi lake, Kanchory alidai kuwa polisi wametumia kukamata kiholela, utekaji nyara, vitisho na unyanyasaji wa waandamanaji, haswa vijana (Gen Z) ambao ni kundi dhaifu linalohitaji ulinzi maalum kwa mujibu wa katiba.

“Nimeona mwombaji amedhihirisha kuwa ombi hilo ni la ubishi na si la kipuuzi. Pili, amedhihirisha kwamba ni kwa manufaa ya umma kwamba amri zinazoombwa zinatolewa,”  Jaji Thande aliamuru.

Uamuzi huo unatumika kama ushindi muhimu kwa haki za binadamu na ujumbe wazi kwamba matumizi ya nguvu zisizo na uwiano dhidi ya waandamanaji wa amani ni jambo lisilokubalika na ni kinyume cha sheria.

Uamuzi huo unajiri huku kukiwa na maandamano yanayoendelea nchini Kenya kupinga nyongeza ya kodi iliyopangwa ambayo wengi wanahofia itazidisha mzozo wa gharama ya maisha.