Babu Owino awataka raia kuripoti wanaposhuhudia wenzao wakitekwa nyara

"Usione Mkenya mwenzetu akitekwa ukatulie, tafadhali ACT. Tumia chochote karibu nawe na umwokoe Mkenya mwenzako"

Muhtasari

•Owino aliwataka Wakenya kuwa macho na kuingilia kati kikamilifu wakati wa utekaji nyara.

•Alisisitiza umuhimu wa kutokuwa watazamaji tu, badala yake, kuchukua hatua za haraka na kukomesha uhalifu huu.

BABU OWINO.
Mbunge wa Embakasi Babu Owino BABU OWINO.
Image: FACEBOOK//BABU OWINO

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amewataka Wakenya kusimama pamoja na kusaidiana wakati wa maandamano yanayoendelea dhidi ya serikali ambayo yamekumbwa na visa vya utekaji nyara na mauaji.

Katika taarifa yake kupitia akaunti yake ya instagram  saa chache baada ya maandamano ya Jumanne, Owino aliwataka wananchi kuchukua hatua dhidi ya utekaji nyara unaoongezeka.

Owino aliwataka Wakenya kuwa macho na kuingilia kati kikamilifu wakati wa utekaji nyara.

Alisisitiza umuhimu wa kutokuwa watazamaji tu, badala yake, kuchukua hatua za haraka na kukomesha uhalifu huu.

Owino alitoa wito kwa raia kutumia njia zozote zinazopatikana kulindana na kukabiliana na watekaji nyara.

Alisisitiza ulazima wa kuchukuliwa hatua kwa pamoja ili kuhakikisha usalama wa Wakenya wote na kuzuia ongezeko la utekaji nyara wa mchana wakati wa maandamano yanayoendelea.

“Wakenya, lazima tukomeshe utekaji nyara wa mchana kwa kutumia nguvu sawa na kinyume ambayo majambazi wanatumia kwa watu wetu."

"Usione Mkenya mwenzetu akitekwa ukatulie, tafadhali ACT."

"Tumia chochote karibu nawe na umwokoe Mkenya mwenzako. Wacha tushughulike na watekaji nyara,” Owino alisema.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR) pia imetaka uchunguzi wa kina ufanywe kuhusu matukio ya hivi majuzi ya kutisha nchini Kenya, ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa miili iliyokatwa viungo na maandamano yanayoendelea.

Julai 16, 2024, KNCHR ilieleza mshtuko na wasiwasi kuhusu kupatikana kwa miili iliyoagwa katika eneo la taka la Kware huko Mukuru Kwa Njenga, Nairobi, ambapo mshukiwa alikiri kuwaua wanawake 42, ingawa ni miili kumi pekee ndiyo imepatikana.

Tume hio pia ilitoa taarifa kuhusu maandamano dhidi ya serikali, ikiripoti vifo 50 na mamia ya majeruhi, ikitaka uchunguzi ufanyike juu ya vifo hivi na matukio ya ukatili wa polisi.

Zaidi ya hayo, KNCHR ilishutumu utekaji nyara, kukamatwa kiholela, na mateso yanayohusiana na maandamano hayo, huku watu 59 wakitoweka na 682 kukamatwa kiholela.

Walimtaka Rais kutekeleza sera ya kutovumilia ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na vyombo vya usalama na kuliomba Bunge na Hazina kufadhili uchunguzi wa mauaji ya kiholela na vifo vya bila kukusudia.