Uhuru wa kweli upo leo, hakuna nafasi ya maumivu na mateso tena - DP Gachagua

Kibwagizo cha 'Uhuru Unakuja' kilikuwa kinatumiwa sana na mrengo wa Kenya Kwanza katika kampeni zao, na sasa ni kama ushafika!

Muhtasari

• Ni wakati wa kufanyia wananchi kazi. Hatuwezi kupoteza dakika yoyote - DP Gachagua.

Gachagua asema Uhuru hatimaye umefika
Gachagua asema Uhuru hatimaye umefika
Image: Facebook

Naibu rais Rigathi Gachagua ameradidi kibwagizo walichokuwa wakikitumia katika kampeni zao kwamba hatimaye, Uhuru uko nasi hapa na kusisitiza kwamba kuteseka na kunyanyaswa kumeshapitwa na wakati sasa katika serikali mpya ya Kenya Kwanza.

Akizungumza katika sherehe za mashujaa zilizoandaliwa kwenye uwanja mdogo wa Uhuru Gardens jijini Nairobi, DP Gachagua alisema kwamba wao kama serikali waliahidi wananchi kwamba watawafanyia kazi na kusisitiza kwamba hawawezi kuchepuka kutoka mkondo huo.

“Ni wakati wa kufanyia wananchi kazi. Hatuwezi kupoteza dakika yoyote. Hakuna nafasi tena ya maumivu na mateso. Uhuru wa kweli upo leo,” Gachagua alisema katika hotuba yake ya muda mfupi huku akimwalika rais William Ruto kutoa hotuba yake ili kuhitimisha kilele cha sherehe hizo.

Katika kampeni zao, muungano wa Kenya Kwanza ulibuni kibwagizo cha ‘Uhuru Unakuja’ ambapo walikuwa wakiwakejeli wenzao kutoka mrengo pinzani kwa kile waliwasuta kuwa ndio chanzo kikubwa cha ugumu wa maisha kwa mwananchi wa kawaida.

Katika kibwagizo chao, Kenya Kwanza walikuwa wananuia kutuma ujumbe kwa Wakenya na wafuasi wao kwamba uhuru wa kiuchumi ambao walisema ulipotea baada ya Handshake ungerejea pindi wangechukua hatamu za uongozi kutoka kwa rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Pia alionekana kugusia suala la kuteswa na maumivu ambapo si mara moja amesikika akisema uongozi uliopota ulimkandia vikali na mpaka kuelezea kwamba aliwahi tolewa nguo mbele ya watoto wake, kitu ambacho alisema hakitawahi tokea kwa Mkenya yeyote katika uongozi wa Kenya Kwanza.