Miguna apata Ksh 45K noti za 1000 za zamani kwenye nyumba yake, ataka serikali kumfidia

Mwanasheria huyo alililia AG Muturi kutoa agizo la benki kuu ya Kenya kumfidia kwani alifurushwa hadi kukosa nafasi ya kuzibadilisha.

Muhtasari

• Dikteta huyo baadaye alibadilisha noti za Sh 1000 na kuweka mpya. Ningependa AG Muturi abadilishe noti zangu za zamani na kunipa mpya - Miguna.

Miguna Miguna afunguka kilichosababisha kufurushwa nchini 2018
Miguna Miguna afunguka kilichosababisha kufurushwa nchini 2018
Image: Facebook

Wakili Miguna Miguna ambaye alirejea humu nchini hivi karibuni baada ya kufurushwa kwa lazima nchini mnamo mwaka 2018 anazidi kukadiria hasara baada ya kurudi na kupata noti za kitambo katika moja ya rafu zake.

Miguna Miguna alielezea kuwa alilazimishwa kuondoka kwa nguvu, hatua ambayo haikumpa nafasi hata kidogo kufanya mambo yake na katika mchakato huo ndipo alisahau bunda lake na noti za elfu moja moja hadi kiasi cha elfu 45.

Baadae mwaka 2019 serikali ya Kenya chini ya uongozi wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta ilitoa agizo la kubadilishwa kwa noti hizo za zamani na noti mpya za elfu moja zikaanza kutumiwa hivyo kufanya zile za zamani kutokuwa halali katika biashara yoyote nchini Kenya.

Wakili huyo ambaye amehasimiana na kinara wa ODM Raila Odinga sasa anakadiria hasara baada ya kurudi na kupata noti hizo zenye thamani ya elfu 45 nyumbani kwake.

Anamtaka mwanasheria mkuu wa serikali mpya Justine Muturi kutoa agizo lake kufidiwa kwa kubadilishiwa na noti mpya katika benki kuu ya Kenya.

“Wakati dhalimu Uhuru Kenyatta alipanga njama na Raila Odinga ili kunifurusha nchini kwa nguvu, walisambaratisha vitu katika nyumba yangu, wakaniteka na kuniweka kizuizini, nilikuwa na Ksh 45000 mfukoni. Dikteta huyo baadaye alibadilisha noti za Sh 1000 na kuweka mpya. Ningependa AG Muturi abadilishe noti zangu za zamani na kunipa mpya,” Miguna alilia.

Wakili huyo baada ya kukaa uhamishoni zaidi ya miaka 4 kwa kushindwa kusafiri kuja nchini kutokana na vizuizi, serikali ya rais Ruto iliviondoa vizuizi vyote na kumwezesha kurudi nchini ambapo alitua JKIA mnamo Oktoba 20.