Uchunguzi wa mwili wa Mwingereza aliyeuawa na 'jini' Mombasa umekosa kubaini chanzo

Raia huyo wa Uingereza alifariki mwaka 2020 na mwili wake ulifukuliwa wiki jana kufanyiwa uchunguzi wa kubaini chanzo cha kifo chake.

Muhtasari

• Luftunisa Kwandwalla, 44, alikuwa amezuru Mombasa ambapo alifariki na mwili wake kuzikwa siku moja baadaye.

Maziara
Maziara
Image: The Star

Mwaka 2020 taarifa za kifo cha kutatanisha cha raia mmoja wa Uingereza aliyefariki Mombasa zilisambaa, haswa baada ya watu wa karibu kudai kuwa aliuawa na jinni.

Mahakama ilitoa kibali cha mwili huo kufukuliwa ili kufanyiwa uchunguzi zaidi ambapo siku chache zilizopita matokeo ya uchunguzi huo yalitoka  na kilichoshangaza zaidi ni kwamba uchunguzi huo ulishindwa kubaini kilichomuua mwanamke huyo raia wa Uingereza.

Luftunisa Kwandwalla, 44, alikuwa amezuru Mombasa ambapo alifariki na mwili wake kuzikwa siku moja baadaye, jambo ambalo familia yake kutoka Uingereza ilidai kulikuwa na mchezo chafu wa kutaka kuficha ukweli wa kilichomuua , na hivyo kutaka uchunguzi kufanyiwa mwili wake.

Kulingana na jarida la Nation, kiongozi wa dhehebu la Kiislamu jijini Mombasa kwa jina Arif Mohammed Iqbal ambaye pia alijitangaza kama mganga alinukuliwa akisema kifo cha mwanamke huyo kilisababishwa na nguvu za gizani.

Uchunguzi wa mwili wake uliofukuliwa wiki iliyopita haukuweza kubaini chanzo cha kifo chake lakini sampuli zilizochukuliwa kutoka kwenye udongo wa kaburi, ikiwa ni pamoja na mabaki ya figo, kibofu cha mkojo na utumbo, zilichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa sumu, kulingana na ripoti iliyotolewa kwa familia na Mwanapatholojia Mkuu wa Serikali Johansen Oduor.

“Ubongo umesinyaa na kupatikana ndani ya fuvu lililofunguliwa. lilikuwa bado halijaharibika. Chanzo cha kifo hakijajulikana ikisubiri histolojia, vipimo vya sumu na DNA,” nukuu ya sehemu ya ripoti hiyo.

Cheti cha kifo kilichotolewa na serikali mnamo 2020 kiliorodhesha sababu yake ya kwanza ya kifo kama kufeli kwa moyo na mapafu.