Viwanda vya pombe haramu vifungwe, hatutakubali taifa letu liundwe na walevi - rais Ruto

Ruto aliwataka polisi na waratibu wa mikoa wote kuhakikisha viwanda vyote vya pombe haramu vimefungwa mara moja.

Muhtasari

• Tuna vinywaji vya kutosha vilivyosanifiwa na serikali na ambavyo ni salama kwa matumizi - Ruto.

Rai atoa amri ya kufungwa kwa viwanda vya kuuza pombe haramu
Rai atoa amri ya kufungwa kwa viwanda vya kuuza pombe haramu
Image: Facebook, Maktaba

Rais William Ruto ameapa kuhakikisha vilabu vyote na maeneo yanayouza pombe haramu kufungwa mara moja.

Akizunguma Ijumaa kwenye kaunti ya Mombasa, rais alisema kuwa maeneo kama hayo yanayoendeleza biashara ya pombe haramu yamewapoteza wanaume wengi ambao ni nguvu kazi ya taifa.

Alitoa wito kwa wasimamizi kufungia viwanda vyote vya kusindika pombe haramu.

"Nimesema tutafunga, na wasikie haya, hatutakubali taifa letu liundwe na walevi, inabidi tufikirie tutafanya nini. Kwa askari wetu wote kutoka polisi na waratibu wa mikoa, lazima tuhakikishe kuwa kila mahali ambapo pombe haramu inatengenezwa kunafungwa,” alisema.

Kulingana na Ruto, pombe iliyoidhinishwa inatosha na ni salama kwa matumizi, hivyo basi kuna haja ya kuziba sehemu hizo haramu.

"Tuna vinywaji vya kutosha vilivyosanifiwa na serikali na ambavyo ni salama kwa matumizi. Inatosha na watengenezaji wanalipa ushuru. Vile haramu vinatudhuru kwani hawatoi ushuru, na wakati huo huo kuwahatarisha Wakenya. ," aliongeza rais.

Haya yanajiri siku chache baada ya mamlaka katika kaunti za Mlima Kenya mashariki kuelezea wasiwasi wao kuhusu ongezeko la kutisha la aina mpya ya pombe haramu ambayo imeingia kwenye baa.

Kulingana na vyanzo vya habari, pombe hiyo hutengenezwa kwa unga wa mtama na kisha kubadilishwa kuwa chakula cha mifugo kabla ya kuingizwa kwenye sehemu za burudani kwa ajili ya kuuzwa.

Ikumbukwe rais Ruto tangu awali aliweka wazi kutofurahishwa kwake na vilevi humu nchini huku akidoeza kuwa yeye hawezi onja hata kidogo.

Mapema alipoapishwa, aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko alizua utani mitandaoni akisema kwamba rais ameibadilisha ikulu kuwa sehemu ya kunywa maji na chai tu na hata kuapa kuanza kujizuia kiwango cha pombe ambacho alikuwa anakunywa.