Kasisi wa Katoliki ataka baadhi ya makanisa kufungwa, "Yana kelele kuliko baa za pombe"

Hatua inayofuata iwe ni kufunga makanisa katika makazi kwa sababu kwa nini watu waabudu kwa kelele nyingi - Fr Kinyua alisema.

Muhtasari

• Makanisa yetu yana kelele nyingi kuliko baa za kunywa. Hiyo inakuambia tuna tatizo,” aliongeza.

Kasisi Charles Kinyua
Kasisi Charles Kinyua
Image: Facebook

Huku kukiendelea kuwa na gumzo pevu mitandaoni kuhusu hatua ya serikali ya kaunti ya Nairobi kuangusha mjeledi kwa sehemu za starehe zilizopo karibu na makazi, baadhi ya watu wamekuwa pia wakisukuma mjeledi kama huo kuangushwa kwa sehemu za ibada zinazohubiri kwa sauti za kukera.

Kasisi mmoja wa kanisa la Kikatoliki kwa jina Charles Kinyua amekuwa wa hivi punde kutilia neno katika gumzo hilo kwa kusema kuwa kuna haja maeneo ya kuabudu pia kudhibitiwa katika sauti ambazo wanazipiga wakati wa mahubiri yao.

Katika video moja ambayo alipakia Tiktok, kasisi Kinyua alisema kuwa nchi yetu imejawa na kelele zisizo za maana na kuwa aliunga hatua hiyo mkono kwa asilimia mia.

“Nchi yetu imejaa kelele. Juzi kuna bwana mmoja humu nchini, mwanasheria ambaye pia ni  mwanasiasa kutoka kaunti hii ya Turkana. Alitoa kauli ambayo niliiunga mkono kwa asilimia 100. Haya ndiyo aliyoyasema kwamba, kwa vile baa zimezuiwa kufanya kazi katika makazi kwa sababu ya kelele, hatua inayofuata iwe ni kufunga makanisa katika makazi kwa sababu kwa nini watu waabudu kwa kelele nyingi? Je, watu hawawezi kuabudu wakiwa kimya?” kasisi huyo alisema.

"Niliweza kuona jinsi wanafiki walivyokuwa wakimtuhumu ... hapana unafikiri kama mpagani, asiyeamini Mungu ... lakini mtu huyo alikuwa na hoja. Leo, makanisa yana kelele kuliko baa, huo ndio ukweli. Makanisa yetu yana kelele nyingi kuliko baa za kunywa. Hiyo inakuambia tuna tatizo,” aliongeza.

Kwa miezi kadhaa sasa kumekuwa na mjadala huo wa kufungwa kwa baadhi ya baa zinazopiga kelele, mjadala ambao ulianzishwa na diwani wa Kileleshwa, Robert Alai.

Wiki iliyopita, Gavana Sakaja alifuta leseni zote za vilabu vya usiku na maduka ya pombe ndani ya maeneo ya makazi, akisema hakuna leseni zingine zitatolewa au kuongezwa kwa waendeshaji wa biashara hizo katika makazi ya jiji.

Wikendi pia rais Ruto alimtaka Sakaja kuendeleza vita vyake dhidi ya baa ambazo zinapiga kelele za kukera katika maeneo na mitaa ya makazi ya watu wa Nairobi.