Babu Owino: Jumuisha Hustler Fund, elfu 6 ya Raila na Kazi Mtaani, patia kila hasla 100K

Owino alisema pesa hizo zinafaa kutolewa kama ruzuku na wala si kama mkopo wa kurejeshwa na riba.

Muhtasari

• "Mimi nataka kumwaambia kuwa hizi ni pesa za wananchi na sharti wapewa bila kutakiwa kuzirudisha,” Owino alisema.

Babu Owino na William Ruto,Rais
Babu Owino na William Ruto,Rais
Image: Facebook

Mbunge wa Embakasi East Babu Owino amemtaka rais William Ruto kutotoa pesa za Hustler Fund kama mkopo kwa wananchi bali kuifanya kama ruzuku kwa wapambanaji wa maisha ya chini.

Kulingana na Owino, rais Ruto alitoa ahadi hiyo wakati wa kampeni zake na wala hakusema pesa hizo zitakuwa kama mkopo wa kurudishwa tena kwa riba ya asilimia 8.

Owino anasema pesa hizo ni tozo la wananchi ambalo linafaa kurudi kwao ili kuwawezesha kujikimu katika biashara ndogo ndogo kwani ndio dhima kuu ya mahasla.

“Mawazo yangu kwa Hustler Fund ni kwamba Ruto wakati wa kampeni alisema pesa hizi zilifaa kuwa pesa za bure kwa wanawake na wanaume kuanzia biashara. Sasa hivi wanasema Hustler Fund inalipwa kwa riba ya 8%. Mimi nataka kumwaambia kuwa hizi ni pesa za wananchi na sharti wapewa bila kutakiwa kuzirudisha,” Owino alisema.

Vile vile, Owino alimtaka Ruto kujumuisha pesa hizo za Hustler Fund na zile elfu 6 ambazo Raila Odinga aliwaahidi Wakenya iwapo angeshinda na kuwapatia Wakenya.

Mbunge huyo mtetezi mkali wa Odinga alisema elfu 6 ni pesa ambazo zilikuwa zimeratibiwa na waliziacha kwa mkoba wa serikali.

“Hizi pesa tulikuwa tumezibajetia na ziko kwa hazina kuu. Kwa hivyo ninamwambia rais Ruto kujumuisha pesa hizi za ustawi wa jamii elfu 6, pamoja na zile za Hustler Fund na pia zile za Kazi Mtaani kwa vijana na kuwapa mahalsa wote kiwango cha chini cha laki moja,” Owino alisema.