Alai atofautiana na makampuni ya kamari kuwapeleka 'wacheshi' Qatar

Hoja yake ni kwamba makampuni hayo yangefadhili safari za wachezaji wa timu ya taifa, na si watu mashuhuri wasio na lolote katika fani ya michezo.

Muhtasari

• Makampuni ya kamari yalipaswa kuwapeleka wanamichezo mashuhuri hadi Qatar na sio kukusanya kundi la wavivu wasio na maana ili kuwaendesha kwa shangwe - Alai.

Alai asuta makampuni ya kamari kupeleka wachekeshaji Qatar
Alai asuta makampuni ya kamari kupeleka wachekeshaji Qatar
Image: Facebook

Diwani wa Kileleshwa Robert Alai amekosoa makampuni ya ubashiri na michezo ya bahati nasibu kwa kuwachukuwa watu maarufu wa humu nchini kushuhudia mechi za kombe la dunia nchini Qatar.

Alai kupitia ukurasa wake wa Twitter, alisema kuwa makampuni hayo yangefanya vyema iwapo yangefadhili safari ya watu wanaojishughulisha katika sekta ya michezo kama wachezaji wenyewe kwenda kushuhudia mechi hizo badala ya kuwachukua wachekeshaji na watu wenye ufuasi mkubwa mitandaoni – watu ambao aliwaita kama wenye mzaha tu.

“Makampuni ya kamari yalipaswa kuwapeleka wanamichezo mashuhuri hadi Qatar na sio kukusanya kundi la wavivu wasio na maana ili kuwaendesha kwa shangwe. Je, ingekuwaje Harambee Stars na Starlets wote wangechukuliwa nao hadi Qatar?” Alai aliuliza.

Matamshi ya Alai yanakuja saa chache tu baada ya mwanamuziki KRG the Don pia kuwasuta wachekeshaji ambao walikubali kupelekwa Qatar na makampuni ya Kamari, hatua ambayo aliitaja kama kumdhalilisha Churchill, mchekeshaji mkongwe aliyewainua wengi hadi kupata umaarufu.

Kulingana na the Don, wachekeshaji hao walirundikwa kwenye ndege moja kama shehena ya mizigo ambapo pia walipewa masharti makali dhidi ya kuvua nguo zenye nembo ya kampuni ya Kamari licha ya kuwepo na hali ya jua kali nchini Qatar.

Wanapelekwa Qatar kuwekwa kwa hoteli kidogo kidogo na kuzungukazunguka kuangalia majumba marefu wakicheka tu. Walianza kufanya maigizo ya vichekesho kama kujiliwaza tu,” KRG alisema.

Baadhi walikubaliana na kauli ya Alai huku wengine pia wakipinga kuwa ni jukumu la serikali kufadhili safari za wachezaji wa timu za taifa kuendqa kushuhudia na kupata uzoefu wa mechi kama zile.

“Hapana serikali ilipaswa kuipeleka timu ya taifa Qatar sio wabunge na viongozi wa serikali. Kampuni za kamari ziko katika biashara zao na hazijawahi kufanya kampeni ya kufufua hali ya michezo nchini,” mmoja alimwambia.

“Mawazo yangu haswa, inapaswa kuwa ama wanamichezo wetu au wateja wao waaminifu. Wanablogu hao na "waundaji wa maudhui" waliongeza thamani ndogo sana kwa maoni yangu,” mwingine aliungana naye.