KRG: Wachekeshaji wako 'desperate' kupelekwa Qatar kama mizigo kwa ndege moja, aibu!

Mtu unapelekwa Qatar na kurudishwa siku 2, ndio kusema huwezi kuwa hata na pesa zako ujiongengee kukaa huko? - KRG aliuliza.

Muhtasari

• Wanapelekwa Qatar kuwekwa kwa hoteli kidogo kidogo na kuzungukazunguka kuangalia majumba marefu wakicheka tu - KRG aisema.

KRG the Don
KRG the Don
Image: Instagram//KRG

Mwanamuziki anayejidai kuwa tajiri zaidi nchini Kenya KRG the Don ameangusha mjeledi wa moto kwenye migongo ya wachekeshaji wa Kenya ambao walifadhiliwa na baadhi ya makampuni za ubashiri na bahati nasibu kwenda kutazama mechi za kombe la duni Qatar.

KRG alisema kuwa wachekeshaji hao ambao wengi waliinuliwa hadi kupata umaarufu na mchekeshaji wa muda mrefu Mwalimu Churchill walilichafua jina la Churchill pamoja na juhudi zote kwa kukubali kufadhiliwa.

Alisema kuwa walirundikwa kwenye ndege moja kama gunia za viazi mbatata ili tu kuenda Qatar na licha ya nchi hiyo kuwa na joto kali, walilazimishwa kuvalia masweta mazito yenye nembo za makampuni hayo mradi tu kutangaza biashara yao ya ubashiri.

“Naihurumia tasnia yetu ya vichekesho 😂😂😂 @mwalimchurchill lazima atahuzunika sana baada ya bidii na wakati aliowekeza kwenu wavulana mnamwangusha. Wale watu tulikuwa na imani nao, walipata kazi za Netflix, wengine walikuwa wanafanya standup comedy, wanapelekwa Qatar kuwekwa kwa hoteli kidogo kidogo na kuzungukazunguka kuangalia majumba marefu wakicheka tu. Walianza kufanya maigizo ya vichekesho kama kujiliwaza tu,” KRG alisema.

Msanii huyo anayejiita Bilionea alisema kuwa wasanii hao waliwekwa kwenye upeo wa kiwanja ambako hata hawangeweza kuona wachezaji uwanjani vizuri kwani huko juu ni mbali sana kutoka sakafuni ambapo wachezaji wanakitifua.

“Halafu mnasema ati ni ustaa, ustaa ni kuwa mtu aliyekata tamaa hivyo? Yaani unapelekwa kwa nchi ya mwenyewe na unarudi baada ya siku mbili, ndio kusema kuwa hata wewe huwezi kuwa na pesa yako ya kujiongeza haya ukae siku zingine zaidi?” The Don aliuliza.