Rais Museveni akataa ushawishi na kampeni zozote za kutaka kuhalalishwa kwa LGBTQ

"Natamka tena, msijaribu kuleta huo upuzi huku kuhusu mambo hayo tafadhali" - Museveni.

Muhtasari

• Alisema wakati wa kongamano la Washington, Wamarekani hawakujaribu kuibua suala la LGBTQ sababu wangekosana.

Image: BBC

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesisitiza tena kuwa taifa lake haliko tayari kuketi chini na kuwa na mazungumzo ya aina yoyote kuhusu jamii ya watu wanaofagilia mapenzi ya jinsia moja.

Rais huyo ambaye alikuwa akizungumza katika runinga moja ya nchini Uganda, alikashfu vikali vitendo vya wanachama wa LGBTQ huku akisema kuwa huo ni upuzi ambao hauna nafasi hata kidogo katika taifa lake.

Aliwataka Waganda kutojaribu kuzua mjadala wa kutaka kuhalalishwa kwa mapenzi ya jinsia moja huku akisema kuwa mwishoni mwa mwaka jana marais wa Afrika walipokongamana jijini Washington Marekani,, Wazungu hawakujaribu kuzua mjadala huo kama ilivyo kawaida yale.

Alisema kuwa Wazungu walijua kuwa wangeanzisha mjadala kuhusu kuhalalishwa kwa LGBTQ Afrika, huo ndio ungekuwa mwisho mwa mkutano wao na hivyo waliamua kuzungumzia suala kuu lililowapeleka kule – biashara.

“Mimi ni Yoweri Museveni, Yoweri ni jina la Kiyahudi kutoka ukoo wa beshert na natamka tena, msijaribu kuleta huo upuzi huku kuhusu mambo hayo tafadhali. Tulikuwa Washington na safari hii Wamarekani waliandaa kongamano vizuri, hawakuleta mjadala wa LGBTQ, kwa sababu tungeahirisha mkutano wetu na wao. Walibaki katika njia kuu ya kujadili biashara, ambayo ilikuwa vizuri. Wangejaribu kuleta tu mjadala kama huo tungekuwa na shida nao,” Museveni alisema.

Tamko la Museveni linajiri kipindi ambapo nchini Kenya kumeibuka mjadala mkubwa kuhusu LGBTQ haswa kufuatia kifo cha mwanaharakati wa jamii hiyo Edwin Chiloba aliyezikwa siku mbili zilizopita.

Kifo chake kilizua gumzo kubwa duniani mpaka Marekani kutoa tamko la kutaka kujumuishwa katika uchunguzi wa kifo chake ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka.

Itakumbukwa miaka kadhaa iliyopita wakati rais mstaafu Uhuru Kenyatta alitembelea Marekani, alikabiliwa na suala la iwapo ako tayari kuhalalisha LGBTQ nchini, jambo ambalo Kenyatta alilipuuzilia mbali vikali na kusema ni kinyume na mila, miiko, desturi na tamaduni za Wakenya.

Pia mwaka jana rais Ruto katika ziara yake alikabiliwa na swali kama hilo naye akasisitiza msimamo wa mtangulizi wake akisema kuwa Kenya inakabiliwa na changamoto nyingi sana zinazohitaji kutafutiwa suluhu la kudumu na wala hakuna nafasi ya kuketi kuanza kujadili mambo ambayo aliyataja kuwa kinyume na tamaduni zetu.