Dalali atangaza kuuza chupi za mume na mkewe baada ya kukataa kulipa kodi ya nyumba

Wapangaji hao walikuwa wamekodisha nyumba hiyo na kodi yao ilifikia Ksh 120K ambayo walishindwa kulipa, nguo zao zikafungiwa ndani.

Muhtasari

• Dalali huyo aliweka tangazo kwenye jarida moja la humu nchini akitaka umma kujitokeza ili kuweka maombi ya kununua nguo hizo zilizopigwa tanji.

• Kodi ya wapangaji hao ilikuwa imefika kiasi cha elfu mia moja na ishirini pesa za Kenya.

Dalali atangaza kuuza chupi za wapangaji waliokosa kulipa kodi
Dalali atangaza kuuza chupi za wapangaji waliokosa kulipa kodi
Image: Facebook

Tangazo la madalali wa kupiga mnada mali zilizopigwa tanji katika kaunti ya Kisumu limezua kicheko kwenye mitandao ya kijamii baada ya kampuni moja ya madalali kwa jina Nyaluoyo kutangaza kupiga mnada vitu mbalimbali katika  nyumba ya mpangaji mmoja aliyekwama kulipa kodi ya nyumba hiyo.

Madalali hao wa Nyaluoyo waliweka tangazo la kupiga mnada mali hiyo kwenye gazeti la Jumatatu Januari 30. Baadhi ya mali ambayo madalali hao walitangaza kupiga mnada ni pamoja na chupi za mwanamume na mwanamke waliokuwa wamepangisha katika nyumba hiyo.

Nyaluooyo walitoa wito kwa umma kujitokeza ili kuweka maombi yao ili kuuziwa chupi hizo, zikiwemo 4 za mwanamume, 4 za mwanamke, mabegi mawili ya watoto, miongoni mwa vitu vingine.

Tangazo hilo lilikuwa linasema kuwa ni mzozo uliokuwa kati ya mmiliki wa nyumba na mpangaji wake kwa jina Zacharia Sichenje Masika.

Yeyote ambaye alitaka kuuziwa mali hiyo iliyopigwa tanji kutoka kwa mpangaji mkaidi alitaarifiwa kujitokeza katika ofisi za kampuni hiyo ya madalali mnamo Februari 7 saa tano asubuhi katika kaunti ya Kisumu.

Tangazo hilo lilionekana kwenye jarida moja la Jumatatu na wengi walilitupia vijembe kwa utani mwingi, wakisema kuwa hiyo ilikuwa kama njia moja ya kumdhalilisha mpangaji huyo na familia yake kwani hakuna mtu anayeweza kujitokeza kununua chupi zilizotumiwa wakati mpya sokoni huuzwa hadi kwa bei ya jioni ya shilingi mia tu.

Inasemekana kuwa mpangaji huyo alikuwa amekodisha chumba kimoja jijini Kisumu ambapo alikuwa anakitumia kama duka la kuuza nguo na malimbikizi ya kodi ya kila mwezi yalikuwa yamefikia laki moja na elfu ishirini ambayo alishindwa kulipa na mali yake yakapigwa tanjia alipofungiwa nje.