Kisa cha 'mama wa kanisa' aliyewaua watoto wake 2 na kuwazika ili kumfurahisha Mungu

Polisi walifanikiwa kumuokoa mtoto wa 3 ambaye alisimulia jinsi mama yao aliwatesa ndugu zake kwa njaa na kuwafungia hewa safi ya kupumua hadi wakafariki.

Muhtasari

• Mahakama iliamuru miili ya watoto hao kufukuliwa kwa uchunguzi zaidi kufuatia kifo chao kabla ya mashtaka kuanza.

• Watoto hao wawili walizikwa kati ya Machi 16 na 17 katika kaburi lisilo na kina kirefu.

crime scene
crime scene

Polisi wanamshikilia mwanamke mmoja kaunti ya Kilifi baada ya kudaiwa kuwatesa njaa watoto wake kabla ya kuwaziba wasipate hewa safi ya kupumua hadi kufa ili kumfurahisha Mungu.

Polisi Jumatano jioni pia walimkamata mwinjilisti mwenye utata kutoka Kaunti kuhusiana na kifo cha watoto hao wawili katika kijiji cha Shakahola.

Mwinjilisti huyo wa kanisa la Good News International yuko chini ya ulinzi wa polisi baada ya mahakama ya Malindi kuamuru kufukuliwa kwa miili ya watoto hao. Wengine walioorodheshwa kuwa washukiwa wa kifo cha watoto hao ni wazazi wao Bw Isaac Ngala na Bi Emily Kaunga, jarida moja la humu nchini liliripoti.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), watoto hao wanasadikiwa kufa njaa na baadaye kuzidiwa na mama yao hadi kufa kwa nia ya kuwa ‘mashujaa mbele ya Mungu baada ya kifo’.

Mama huyo ni mwabudu katika kanisa la mchungaji Mackenzie wa kanisa hilo.

“Kulingana na afisa wa uchunguzi Joseph Yator kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai Malindi, polisi walifanikiwa kumuokoa mtoto wa tatu. Mtoto aliyeokolewa alisimulia mateso waliyopitia ndugu zake wawili baada ya njaa kwa muda kabla ya mama yao kuwazibia hewa safi hadi kufa,” DPP alisema.

Watatu hao ambao ni wqazazi wa watoto na mchungaji wanashukiwa kuwazika watoto hao wawili mnamo Machi 16 na 17, mtawalia, katika kaburi lisilo na kina kirefu katika kijiji cha Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Polisi sasa waliamuru kufukuliwa kwa miili ya watoto hao kwa uchunguzi Zaidi kabla ya wazazi na mchungaji kufunguliwa kesi ya mauaji.