Wanafunzi 140,000 wa vyuo wamekosa kupata mikopo huku HELB ikiishiwa pesa

Wanafunzi hao ambao wengi wao ni wa mwaka wa kwanza watalazimika kutafuta njia mbadala za kulipia karo, malazi na matunzo yao.

Muhtasari

• Idadi ya wanafunzi wanaofadhiliwa na serikali katika vyuo vikuu vya umma imeongezeka kwa kasi zaidi katika miaka mitano, jarida moja lilibaini.

• HELB walikuwa wamewasilisha bajeti ya bilioni 4.5 kwa hazina ya kitaifa, bajeti hiyo imekamilika na sasa wanataka bilioni 5.7

Wanafunzi 140k wakosa ufadhili wa HELB
Wanafunzi 140k wakosa ufadhili wa HELB
Image: STAR

Wanafunzi takriban laki moja na elfu 40 wamekosa kupokea mikopo ya kufadhili masomo ya elimu ya juu HELB baada ya bodi hiyo kudai kuwa wameishiwa na pesa hizo za kugawa kwa wanafunzi.

Afisa mkuu mtendaji wa HELB Charles Ringera Jumatano wiki hii aliiambia kamati ya bunge kuhusu elimu kwamba bodi hiyo imeishiwa na pesa za kugawia wanafunzi na hivyo takriban wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo anuwai 140,000 huenda watalazimika kusubiri Zaidi hadi pale wizara ya fedha itakapoachilia pesa hizo.

"Hivi sasa tuna wanafunzi 140,000 wa Tvets na vyuo vikuu ambao hatujaweza kuwafadhili hadi Shilingi bilioni 5.7 kwa sababu tumeishiwa na bajeti tuliyowasilisha kwa Hazina ya fedha ya Shilingi 4.5," Charles Ringera.

Kucheleweshwa kwa malipo kunamaanisha kuwa wanafunzi hao ambao wengi wao ni wa mwaka wa kwanza watalazimika kutafuta njia mbadala za kulipia karo, malazi na matunzo yao huku wakisubiri ufadhili wa serikali.

Bw Ringera alibainisha ombi la kuziba nakisi ya sasa ya ufadhili kupitia bajeti ya ziada lilikataliwa.

Helb inapaswa kuwa hazina inayozunguka ambapo walengwa ambao wamemaliza masomo hulipa ili kusaidia kikundi kipya cha wanafunzi – jambo ambalo limeshindwa kuzaa matunda kwani wengi wa wanaomaliza masomo wamesalia bila kazi na ni vigumu wao kuanza kufanya malipo kwa HELB.

Helb imejitahidi kwa miaka mingi kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya mikopo. Idadi ya wanafunzi wanaofadhiliwa na serikali katika vyuo vikuu vya umma imeongezeka kwa kasi zaidi katika miaka mitano, jarida moja lilibaini.