Hata kama tunaandamana, ni lazima tukemee uharibifu wa mali ya kibinafsi - Gideon Moi

Moi alikemea kuchomwa kwa kanisa na msikiti katika eneo la Kibera Jumatatu usiku.

Muhtasari

• Aliwataka Wakenya kudumisha usalama wa mali ya binafsi hata kama wanaendelea kutumia uhuru wa kikatiba kuandamana.

Moi anyooshea kidole cha lawama vurugu za Kibera
Moi anyooshea kidole cha lawama vurugu za Kibera
Image: Facebook, Maktaba

Mwenyekiti wa chama cha KANU, Gideon Moi amekuwa mwanasiqasa wa hivi punde kukemea uharibifu wa mali uliotokea Jumatatu wakati wa maandamano ya kitaifa yaliyoongozwa na kinara wa Azimio, Raila Odinga.

Moi alizungumzia haswa uharibifu ulioshuhudiwa mtaa wa mabanda wa Kibera ambapo maeneo ya kuabudu kwa Wakristo na Waislamu yaliharibiwa kwa kuchomwa moto.

Seneta huyo wa zamani wa Baringo alikashifu kitendo hicho akisema kwamba Kenya ni nchi ambayo inatambua uwepo wa Mungu kwenye katiba na kitendo cha kuchoma na kuharibu maeneo ya kuabudu ni picha mbaya katika taifa hilo, sawa la kuibaka katiba ya mwaka 2010.

“Lazima tuelewane kama taifa kwamba mielekeo yetu tofauti ya kisiasa isigeuke na kuwa chuki ya kidini kama ilivyoshuhudiwa hivi majuzi katika baadhi ya maeneo ya Eneo Bunge la Kibra, Kaunti ya Nairobi. Katiba yetu inakubali ukuu wa Mwenyezi Mungu katika Dibaji na uhuru wa dini, na hivyo kusisitiza umuhimu wa uvumilivu wa kidini licha ya imani zetu,” Moi alisema.

Mwanasiasa huyo alisisitiza haja ya kuwepo kwa utulivu hata wakati wa maandamano hayo, akisema kwamba kila Mkenya anajukumika kukemea uharibifu wa mali ya kibinafsi.

“Zaidi ya hayo, hata tunapotumia haki ya kuandamana chini ya Kifungu cha 37, ni lazima sote tuwe na msisitizo katika kukemea uharibifu wa mali ya kibinafsi katika sehemu yoyote ya nchi hii, iwe ni kibanda, duka, maduka makubwa au hata shamba,” Moi alishauri.

Jumatatu, mali ya wananchi mbalimbali yaliharibiwa kwa kuchomwa na kuibiwa kaitka sehemu tofauti Nairobi.

Ukiachia mbali kanisa na msikiti kuchomwa Kibera, pia uvamizi ulifanyika katika shamba la familia ya Kenyatta Northlands na kuiba mifugo idadi isiyokadirika.

Pia watu walivamia kampuni ya Odinga iliyoko Industrial Area na kuvunja vioo vya madirisha kwa mawe.