Mabomu mazito ya gavana Susan Kihika yampa ushindi katika vita ya maneno Twitter

"Wewe umefanya awamu ngapi kama gavana?" Kihika alimuuliza jamaa aliyemwambia kwamba atakuwa gavana wa awamu moja tu!

Muhtasari

• “Huu uchungu ni mwingi, chunga usipate shinikizo la juu la damu,” Kihika alimzima mwingine aliyemzomea kuwa ni mlahai wa raslimali za kaunti.

Susan Kihika ampiga kumbo jamaa aliyemshambulia Twitter
Susan Kihika ampiga kumbo jamaa aliyemshambulia Twitter
Image: Twitter

Usiku wa Ijumaa, gavana wa Nakuru Susan Kihika aliamua kutokaa kimya wakati watumizi wa mtandao wa kijamii wa Twitter waliamua kumkaba kwenye koo kwa mashambulizi makali.

 Baadhi ya watumizi hao walimjia juu wakimtuhumu kuwa anatumia vibaya rasilimali za kaunti ya Nakuru na kumtaka alonge na kiongozi wake wa chama William Ruto ili kupunguza gharama ya maisha.

Wengine pia walimkaba kwa nguvu wakimzomea hadharani kwamba hatoweza kushinda awamu ya pili kama gavana katika uchaguzi wa mwaka 2027.

Lakini safari hii, gavana aliweka kando stara yake na kujibu mipigo ambapo wengi walifurahishwa na majibu yake yaliyowatokomeza wakosoaji wake gizani kusikojulikana.

“Gavana wa awamu moja,” Koskei Kisitei alimwambia.

“Wewe umefanya awamu ngapi kaka?” Kihika alimjibu vikali huku akimaliza kwa kicheko.

Baadhi wakiongozwa na gavana wa Nairobi Johnson Sakaja walibaki wakicheka tu kwa majibu makali ya gavana Kihika huku wengine wakisema kuwa jibu kama hilo haliwezi kumpa nguvu Kisitei kujikusanya kwa mipigo upya.

Ushenzi ndo mingi na nyinyi maghasia ya wezi wa rasilmali ya wakenya, ambia Ruto arudishe bei ya unga chini ama atoke kwa kiti ya mwenzake, wezi nyie,” mmoja mwenye hasira zilizopitiliza alimwambia Kihika.

“Huu uchungu ni mwingi, chunga usipate shinikizo la juu la damu,” Kihika alizima kiberiti hicho.

Kihika hivi majuzi amepata afueni ya muda ambapo mahakama ya Nakuru ilimtaka kufika tarehe 18 Aprili mwenyewe kwa ajili ya kusomewa kifungo kwa kukiuka agizo la mahakama katika uteuzi wa mawaziri wa kaunti ya Nakuru.