Fisi wawili wauawa, mmoja apatikana amefungiwa hirizi mkiani

Wanakijiji waliripoti fisi hao kuwahangaisha ikiwemo kumpora na kumjeruhi mtoto ndipo mafisa wa kusimamia wanyamapori wakafika kuwaua.

Muhtasari

• Afisa wa uhusiano mwema na umma wa shirika la kusimamia wanyamapori alidhibitisha kisa hicho.

Fisi wawili wauawa na mmoja apatikana na hirizi mkiani.
Fisi wawili wauawa na mmoja apatikana na hirizi mkiani.
Image: Millard Ayo//Twitter

Jambo lisilo la kawaida lilishuhudiwa katika kijiji cha Nzola wilaya ya Magu mkoani Mwanza kaskazini magharibi mwa taifa jirani la Tanzania baada ya fisi wawili kuuawa na mmoja wao akapatikana na kile wakaazi walisema ni hirizi katika mkia wake.

Kwa mujibu wa Ayo TV, maafisa wa usimamizi wa wanyamapori nchini humo walitumwa kuwadhibiti fisi hao baada ya mwendelezo wao wa kuwashambulia wanakijiji wa eneo hilo.

Afisa wa uhusiano mwema na umma wa mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori nchini humo Vicky Kamata aliiambia Ayo TV kwamba walipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu usumbufu wa fisi ambao walikuwa wanawapora watoto katika kijiji cha Nzola.

Askari hao wa kudhibiti wanyamapori walifika na kufanikiwa kuwaua fisi wawili lakini wananchi walipigwa na butwaa fisi mmoja kupatikana amevalishwa kitu kilichokisiwa kuwa hirizi mkiani.

“Tarehe 24/4/2023 Ofisi ya Detach Mwanza ilipokea taarifa ya Fisi kupora Mtoto na kumjeruhi katika Wilaya ya Magu, Kata ya Nsola Kijiji cha Nsola ambapo Kikosi cha Askari watatu kilienda katika Kijiji hicho kudhibiti Fisi hao. Askari hao walifanikiwa kuwaua Fisi wawili na mmoja kati ya Fisi hao amekutwa na hirizi kwenye mkia kama inavyoonekana kwenye picha,” Kamata alinukuliwa akisema.

Ni kisa ambacho kimewaacha wanakijiji katika hali ya taharuki wasijue cha kufanya, huku sasa ikikisiwa kuwa huenda fisi hao walikuwa wanatumika katika ushirikina na uchawi katika taifa hilo ambalo asilimia kubwa ya wananchi wanaamini katika waganja wa kiasili na visa vya ushirikina.