Binti wa Mugabe ajikuta katika mgogoro wa talaka wa dola milioni 80

Kesi ya talaka kati ya binti ya Mugabe na mumewe imetoa taswira ya utajiri wa ajabu uliokusanywa na familia hiyo

Muhtasari

•Bona Mugabe, 33, aliwasilisha maombi ya talaka ya kuachana na rubani wa zamani wa shirika la ndege Simba Mutsahuni Chikore mwezi Machi.

•Wazimbabwe wamepokea kwa mshtuko na hasira taarifa za kiwango cha utajiri uliokusanywa na mtoto mmoja tu wa Bw Mugabe.

akiwa na wazazi wake kwenye sherehe ya kuhitimu chuo kikuu nchini Singapore mwaka 2013
Bona Mugabe akiwa na wazazi wake kwenye sherehe ya kuhitimu chuo kikuu nchini Singapore mwaka 2013
Image: BBC

Kesi ya talaka kati ya binti ya aliyekuwa Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe na mumewe imetoa taswira ya utajiri wa ajabu uliokusanywa na familia hiyo - ikiwa ni pamoja na nyumba za thamani ya karibu dola milioni 80 (£64m).

Bona Mugabe, 33, aliwasilisha maombi ya talaka ya kuachana na rubani wa zamani wa shirika la ndege Simba Mutsahuni Chikore mwezi Machi, na kuomba kugawanywa kwa mali kushughulikiwa katika kesi tofauti mahakamani.

BBC imeona nyaraka za mahakama zilizowasilishwa na Bw Chikore tarehe 28 Aprili kujibu zile za Bi Mugabe.

Anadai ulezi wa pamoja wa watoto watatu wa wanandoa hao na sehemu ya mali, ambayo ni pamoja na mashamba yasiyopungua 21, ambayo baadhi yalichukuliwa na familia ya Mugabe wakati wa unyakuzi wa mashamba ya wazungu takriban miongo miwili iliyopita, na licha ya serikali kuwa na sera ya "mtu mmoja shamba moja".

Bw Chikore pia anaorodhesha mali 25 za makazi ikiwa ni pamoja na jumba la kifahari huko Dubai - lenye thamani ya jumla ya karibu dola milioni 80, magari ya kifahari, vifaa vya kilimo na mamia ya maelfu ya dola taslimu.

Anasema mali hizo walizipata kibinafsi na kwa pamoja wakati wa ndoa yao, kupitia mirathi na michango kutoka kwa marehemu rais kwa kazi iliyofanywa kwa niaba yake.

Anaongeza kuwa mali ambayo ameorodhesha ni tone la bahari, ikilinganishwa na mali ambayo Bi Mugabe anamiliki moja kwa moja.

Wazimbabwe wamepokea kwa mshtuko na hasira taarifa za kiwango cha utajiri uliokusanywa na mtoto mmoja tu wa Bw Mugabe.

Akijibu, George Charmba, ambaye alikuwa msemaji wa Bw Mugabe na sasa anahudumu katika ofisi ya Rais Emmerson Mnangagwa, alikanusha kuwa wanandoa hao walikuwa na mashamba 21.

"Ardhi yote ya Kilimo ni ya Serikali, na wakulima wanaitumia kwa MSINGI WA KUKODISHA," aliandika kwenye ujumbe wa Twitter.

Aliongeza kuwa hakuna mtu anayepaswa "kujenga siasa au mabishano kuhusu mashamba 21 yanayodaiwa kumilikiwa na Cde Bona na mumewe aliyeachana naye".

Bona Mugabe akiwa na mumewe kwenye mazishi ya babake mwaka 2019
Image: BBC

Haijulikani ni lini kesi ya talaka - iliyowasilishwa mahakamani katika mji mkuu, Harare - itaisha. Bi Mugabe na Bw Chikore walifunga ndoa katika harusi ya kifahari mwaka 2014 ambayo ilihudhuriwa na wakuu kadhaa wa nchi za Afrika - na ilitangazwa moja kwa moja kwenye televisheni ya taifa.

Mugabe alifariki mwaka wa 2019 akiwa na umri wa miaka 95, ikiripotiwa kuwa bila kuacha wosia.

Ameacha mkewe Grace, Bona, watoto wawili wa kiume na mtoto mmoja wa kambo.

Alikuwa madarakani nchini Zimbabwe tangu wakati wa uhuru mwaka 1980 hadi alipotimuliwa mwaka 2017 na aliyekuwa mpinzani wake, Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa.