Gideon Moi amemmiminia sifa mke wake baada ya harusi ya mwanawe

Huku akimpongeza mwanawe kwa harusi hiyo, Gideon alimtakia yeye na mkewe muongozo na baraka za Mungu.

Muhtasari
  • Katika ujumbe kwa mkewe Zahra, kiongozi wa chama cha Kanu alimshukuru kwa kuhakikisha uchumba wa mtoto wao unafanikiwa.
ZAHRA MOI NA GIDEON MOI
Image: GIDEON MOI/TWITTER

Aliyekuwa Seneta wa Baringo na kiongozi wa chama cha Kanu Gideon Moi amemmiminia sifa mkewe Zahra Moi kwa kumfundisha mtoto wao Kigen Moi maadili mema.

Kigen alifunga ndoa na kipenzi cha maisha yake Rebecca Chepchumba katika hafla ya kibinafsi ambayo ilihudhuriwa na watu wakuu wa kisiasa.

Katika ujumbe kwa mkewe Zahra, kiongozi wa chama cha Kanu alimshukuru kwa kuhakikisha uchumba wa mtoto wao unafanikiwa.

"Ninamsherehekea mke wangu mpendwa Zahra Moi kwa kuwa nguzo ya familia yetu. Yeye ni mrembo, mwenye huruma, mkarimu na anayejitolea kwa kila kitu anachofanya," Gideon aliandika kwenye Twitter.

"Ninampongeza kwa juhudi za kuigwa katika kuhakikisha kuwa sherehe ya uchumba ya mwana wetu Kigen Moi ilifanikiwa."

Huku akimpongeza mwanawe kwa harusi hiyo, Gideon alimtakia yeye na mkewe muongozo na baraka za Mungu.

"Ninajivunia mwanangu Kigen Moi kwa kupiga hatua kubwa katika maisha haya kwa kutafuta mkono wa Rebecca Chepchumba katika ndoa. Hakika, uchumba huu ni mradi mzuri wa kijamii na kiroho uliowekwa na Mungu kuhakikisha uandamani na mwendelezo," Gideon alisema.