Ruto: Mimi namjua Raila sana na ndio maana nilimshinda wakiwa na Uhuru

"Ulisema unanijua eti nitaongea onge halafu ninyamaze, lakini pia mimi nakujua vizuri sana na najua maandamano yako yataishia wapi." - Ruto kwa Odinga.

Muhtasari

• “Mimi nikichaguliwa gharama ilikuwa juu, unga ulikuwa shilingi 230 nimeenda kutafuta mahindi nimeleta sasa unga ndio hiyo imefika 170 na inateremka,” Ruto alisema.

Odinga amtambua Ruto kama rais
Odinga amtambua Ruto kama rais
Image: Facebook

Rais William Ruto kwa mara ya kwanza amezungumza kumjibu kinara wa upinzani Raila Odinga kuhusu maandamano ambayo yamekuwa yakiitishwa na muungano wa upinzani kupinga serikali yake.

Ruto ambaye alikuwa anazungumza katika hafla ya mazishi ya mke wa Dedan Kimathi, Mukami Kimathi huko Nyandarua, alisema kuwa anamjua bwana Odinga ndani na nje na ndio maana alimshinda katika uchaguzi wa mwaka jana licha ya kuungwa mkono na rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta.

Rais alikuwa anajibu tamko la Odinga ambaye alizungumza awali kwamba anamjua Ruto vizuri sana katika njama yake ya kumaliza maandamano kwa kuitisha mazingumzo ya pande zote mbili kupitia mchakato wa bungeni.

“Mimi namjua sana Odinga na ndio nilimshinda akiwa na Uhuru (Kenyatta), na kwa sababu namjua sana najua ataendesha hii maneno yake ya maandamano na najua yataishia wapi… kwa sababu tunajuana wewe unanijua na mimi nakujua tumekubaliana wabunge waongee hayo maneno wacha mimi ning’ang’ane na hii kazi,” Ruto alisema.

Rais pia alizungumza kuhusu gharama ya juu ya maisha ambayo Odinga alizungumzia kuwa kero kwa wananchi akisema kuwa kipindi alichukua hatamu bei ya unga ilikuwa juu lakini yeye amefanya jitihada kuhakikisha kwamba licha ya gharama hiyo kuwa juu, angalau kuna dalili kubwa kwamba imeanza kushuka.

“Mimi nikichaguliwa gharama ilikuwa juu, unga ulikuwa shilingi 230 nimeenda kutafuta mahindi nimeleta sasa unga ndio hiyo imefika 170 na inateremka,” Ruto alisema.

Kiongozi huyo wa taifa alimtania Odinga kwamba kitu pekee ambacho anaweza kumshinda labda ni umri na kuwa na weledi wa historia ya Kenya lakini katika masuala ya kutatua uchumi Odinga hamfikii hata kidogo.

“Kwa historia unaweza kunishinda lakini kwa uchumi hapana, mimi naelewa kabisa. Acha tuambiane ukweli na nashukuru ulisema tuambiane ukweli,” Ruto alisema.