Pasta Ezekiel aomba korti kumruhusu kutoa Ksh 50M Kutoka akaunti zake za benki

Mchungaji huyo ambaye akaunti zake zimepigwa tanji alisema angependa kuruhusiwa kutoa pesa hizo ili kuweza kuendesha huduma za kanisa na shule.

Muhtasari

• Alisema kuwa kufungia akaunti za benki kumesababisha ugumu wa kifedha na vifaa kwa shughuli za Shule ya Kimataifa ya Kilifi na New Life prayer Center & church.

Pasta Ezekiel aitaka mahakama kumruhusu kutoa pesa kwenye akaunti zake.
Pasta Ezekiel aitaka mahakama kumruhusu kutoa pesa kwenye akaunti zake.
Image: Maktaba

Mchungaji Ezekiel Odero anaitaka mahakama kumruhusu kutoa angalau shilingi milioni 50 pekee kutoka kwa akaunti zake ili kuweza kuendeleza huduma za kanisa lake la New Life Prayer Centre pamoja pia na shule huko Mavueni kaunti ya Kilifi.

Odero kupitia kwa mawakili wake, aliitaka mahakama kumruhusu kufanya miamala hiyo, wiki chache baada ya akaunti zake Zaidi ya 15 kupigwa tanji kufuatia uchunguzi unaoendelea dhidi ya kanisa lake kushirikiana na lile la Mchungaji Paul Mackenzie kutoka Shakahola kaunti hiyo ya Kilifi.

Katika maombi yaliyothibitishwa kuwa ya dharura, Ezekiel pia anaitaka mahakama hiyo kupitia upya amri zake za kufungia akaunti yake ya benki kutoka siku 30 hadi 15.

"Akaunti za benki hutumika kama tegemeo la watu wengi wasiojiweza, na kitendo cha kuzifunga kitawaelemea watu hawa, na kuwahukumu kustahimili shida na mapambano," inasomeka hati ya kiapo kulingana na Citizen.

Alisema kuwa kufungia akaunti za benki kumesababisha ugumu wa kifedha na vifaa kwa shughuli za Shule ya Kimataifa ya Kilifi na New Life prayer Center & church.

Mbele ya mahakama ya Milimani, Ezekiel alisema kuwa fedha za uendeshaji wa kanisa na shule haziwezi kusubiri kumalizika kwa siku 30 kama ilivyoagizwa na amri iliyotolewa na mahakama mnamo Mei 8.

"Matatizo ya mtiririko wa pesa yaliyosababishwa na kufungiwa kwa akaunti za Mwombaji yanasababisha athari mbaya kwa wafanyikazi na wanafunzi wanaofadhiliwa na New Life Prayer Center & church na shule ya kimataifa ya Kilifi," anateta.

Mnamo Jumatatu, Jaji wa Mahakama Kuu ya Mombasa Olga Sewe alikataa kutoa maagizo ya kufungia akaunti 15 za benki za Ezekiel akisema mahakama yake haina mamlaka ya kushughulikia kesi hiyo.

Mchungaji huyo anaendelea kuchunguzwa baada ya upande wa mashtaka awali kuiambia mahakama kwamab walidokezewa habari kuwa watu waliokuwa wanafariki katika kanisa lake walikuwa wanasafirishwa kinyemela hadi shamba la Mackenzi huko Shakahola kwa ajili ya maziko.

Pia alihusishwa kufanya biashara ya kuuziana kituo cha runinga na Mackenzie.