Seneta Karen Nyamu adokeza kwa nini kifo cha Jeff Mwathi kitasalia kuwa kitendawili

Seneta huyo ameibua maswali kuhusu jinsi uchunguzi wa kifo cha Jeff Mwathi ulivyoshughulikiwa.

Muhtasari

•Nyamu alibainisha kwamba baada ya tukio la aina hiyo, kila mtu aliyekuwa ndani ya nyumba husika anakuwa mshukiwa.

•"Hakukuwa na kukamatwa kwa mtu hata mmoja, hakukuwa na hadithi kuhusu mazingira yaliyopelekea "kujitoa uhai" kwa Jeff na wale aliokuwa nao. Hakuna hadithi yoyote. Hakuna kitu??," Nyamu alilalamika.

Karen Nyamu na marehemu Jeff Mwathi
Image: HISANI

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu ameibua maswali kuhusu jinsi uchunguzi wa kifo cha Jeff Mwathi ulivyoshughulikiwa.

Jumatano asubuhi, alibainisha kwamba baada ya tukio la aina hiyo, kila mtu aliyekuwa ndani ya nyumba husika anakuwa mshukiwa na pengine wanakamatwa ambapo baadaye wanaachiliwa ikiwa hawatapatikana na hatia.

Nyamu alihoji kwa nini haikuwa hivyo katika kesi ya kifo cha kijana huyo wa miaka 23 aliyeaga takriban miezi mitatu iliyopita.

"Hakukuwa na kukamatwa kwa mtu hata mmoja, hakukuwa na hadithi kuhusu mazingira yaliyopelekea "kujitoa uhai" kwa Jeff na wale aliokuwa nao. Hakuna hadithi yoyote. Hakuna kitu??," Nyamu alilalamika.

Seneta huyo wa UDA alikuwa akitoa maoni kuhusu tukio la hivi majuzi la mwanafunzi aliyefariki baada ya kuanguka kutoka ghorofa moja katika eneo la Ruaka. Watu watano walitiwa mbaroni kufuatia tukio hilo.

Mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 23 alidaiwa kuanguka kutoka orofa ya nane ya jengo hilo siku ya Jumatatu. Iliripotiwa kuwa marafiki watano aliokuwa nao wanachukuliwa kama washukiwa na walizuiliwa katika Kituo cha polisi cha Karuri.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, naibu kamishna wa kaunti ya Kiambaa Peter Maina alisema uchunguzi wa kile kilichotokea kabla ya mwanamke huyo aliyetambuliwa kama Catherine Njeri kufariki umeanza.

"Polisi wameanza uchunguzi. Washukiwa watarekodi taarifa na kuwasaidia wapelelezi kwa maelezo yote watakayohitaji,” alisema.

Alisema watuhumiwa hao watasaidiana na upelelezi kubaini kilichotokea katika jengo hilo lililopo kijiji cha Gacharage.

Katika kisa cha Jeff Mwathi, alifariki baada ya kudaiwa kuanguka kutoka orofa ya kumi ya jengo lililo Roysambu. Alikuwa katika nyumba ya mwimbaji maarufu wa Mugithi DJ Fatxo kabla ya kukutana na kifo chake cha ghafla.

DJ Fatxo alidai kuwa hakuwa nyumbani wakati wa tukio hilo. Alisema alikuwa amemwacha marehemu na wenzake wawili.

"Nilitoka na wanawake watatu. Baadaye kurudi baada ya masaa kadhaa niligundua kuwa Jeff hakuwa ndani ya nyumba na wengine walikuwa, mimi ndiye nilienda na wao kwa kituo cha polisi kuripoti kuwa Jeff ametoweka," alisema.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na mtangazaji Massawe Japanni kwenye Radio Jambo, DJ Fatxo alisisitiza kuwa marehemu alikuwa rafiki yake na kubainisha  kwamba hakuwa na sababu yoyote ya kumdhuru.

"Jeff alikuwa rafiki yangu. Sioni sababu yangu kumuua," alisema.