Katibu wa UDA: Ni kweli maisha yamekuwa magumu, viongozi hawamwambii Ruto ukweli

Malala aliwataja baadhi ya viongozi ambao kila mara wanatembelea Ruto kwenye ikulu na badala ya kumwambia ukweli kuhusu maisha kuwa magumu, wanajiongelea mambo yao pekee kuhusu biashara.

Muhtasari

• “Hata kama unafanya kazi kwa serikali halafu ukuje hapa mbele ya wananchi useme eti gharama ya maisha haiku juu, huo utakuwa ni upumbavu nambari moja" - Malala.

Malala awasuta viongozi kwa kutomwambia Ruto ukweli kuhusu maisha kuwa magumu
Malala awasuta viongozi kwa kutomwambia Ruto ukweli kuhusu maisha kuwa magumu
Image: Facebook

Katibu mkuu wa chama cha UDA, Cleophas Malala amewasuta viongozi wanaofanya kazi karibu na mrengo wa serikali kwa kutomwambia rais Ruto ukweli kuhusu gharama ya ju ya maisha ya wananchi wanaowawakilisha serikalini.

 Akizungumza katika hafla ya mazishi huko Kakamega, Malala alikiri kwamba licha ya kuwa ndani ya serikali ya Ruto kama katibu, lakini pia ni Mkenya na anaamka kila asubuhi kwenda dukani kufanya ununuzi na amegundua kuwa bei za bidhaa muhimu imepanda na maisha kuwa magumu.

“Unajua kuwa ndani ya serikali ni jambo zuri na pia ni jambo gumu sana. Na mimi ni mwananchi wa Kenya hata kama ni katibu mkuu wa UDA, lakini kama mwananchi ambaye naamka asubuhi naenda dukani, najua na nasema ukweli kwamba gharama ya maisha iko juu…” Malala alisema.

Aliwasuta viongozi wanaofanya kazi na serikali kwa kutsema ukweli kuhusu gharama ya maisha akisema kuwa huo ni upumbavu.

“Hata kama unafanya kazi kwa serikali halafu ukuje hapa mbele ya wananchi useme eti gharama ya maisha haiku juu, huo utakuwa ni upumbavu nambari moja. Sababu ukweli wa maneno ni kwamba gharama na maisha iko juu,” alisema.

Seneta huyo wa zamani alisema kuwa suala la gharama ya juu ya maisha si la kuachiwa mtu mmoja kulipatia ufumbuzi bali ni jukumu la kila kiongozi kuhakikisha kwamba wanalipatia ufumbuzi kwa faida ya mwananchi wa kawaida.

Malala aliwasuta baadhi ya viongozi wa Kakamega ambao alisema wanakwenda ikulu kukutana na rais kila mara kwa maswala yao binafsi lakini wakifika kwenye hafla za mazishi wanaisuta serikali badala ya kumwambia Ruto ukweli wa maneno wanapomtembelea Ikulu.

“Mnasema mkifika mahali mnataka kusema ule ukweli kabisa mnaachia hapo. Sababu ukweli wa maneno, haya mambo mnakuja kuongea hapa Ayub Savula, wewe Osotsi, wewe Wangwe, mkikuja kule ikulu sijawahi wasikia mkiambia rais haya maneno. Nyinyi mnakuja hapa kuyaongelea kwa matanga,” Malala aliwasuta akiwataja majina.