Bahati agura Jubilee na kujiunga na UDA, atangaza kuwania ubunge Mathare 2027

Mwimbaji huyo aliweka wazi kwamba amefurahi 'kurudi nyumbani.'

Muhtasari

•Bahati alikaribishwa kwenye UDA  siku ya Jumatano na katibu mkuu wa chama hicho Cleophas Malala pamoja na viongozi wengine.

•Bahati alimshukuru rais Ruto kwa kile alichosema, ameweka mazingira mazuri kwa vijana kujiendeleza humu nchini.

amejiunga na UDA
Bahati amejiunga na UDA
Image: INSTAGRAM// BAHATI

Mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za mapenzi Kelvin Kioko almaarufu Bahati amejiunga rasmi na chama tawala cha UDA.

Bahati ambaye aliwania kiti cha ubunge wa Mathare kwa tiketi ya Jubilee katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana alikaribishwa kwenye UDA  siku ya Jumatano na katibu mkuu wa chama hicho Cleophas Malala.

Katika taarifa yake  ya Jumatano alasiri, aliweka wazi kwamba amefurahi kupiga hatua hiyo kubwa ya kisiasa.

"MWANA MPOTEVU 🙏 NINA FURAHA KURUDI NYUMBANI. NIMEPOKELEWA RASMI NA KATIBU MKUU WA CHAMA CHA U.D.A MHE. CLEOPAS MALALA, VIONGOZI WENGINE NA WANAMUZIKI WENZANGU KATIKA  MAKAO MAKUU," alisema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 30 alimshukuru kiongozi wa chama cha UDA, rais William Ruto kwa kile alichosema, ameweka mazingira mazuri kwa vijana kujiendeleza humu nchini.

Wakati huo huo, alidokeza kwamba atawania kiti cha ubunge wa Mathare kwa tiketi ya chama hicho ifikapo 2027.

Bahati alisindikizwa na mke wake Diana Marua, mwimbaji mwenzake KRG the Don na MC Jessy wakati akipokelewa katika makao makuu ya UDA.  Baada ya kukaribishwa chamani, alivalishwa mavazi ya UDA.

Katika uchaguzi wa mwaka jana, Bahati aliibuka wa tatu katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Mathare huku  Anthony Oluoch wa ODM akichukua ushindi. Billian Ojiwa ambaye aliwania kwa UDA alimaliza katika nafasi ya pili.

Hilo lilikuwa ni jaribio la Bahati la kwanza kuwania kiti cha kisiasa nchini Kenya.

Baada ya uchaguzi huo, alitoweka kwenye vyombo vya habari na mitandao yote ya kijamii huku Wakenya wengi wakikisia kuwa alikuwa amekumbwa na msongo wa mawazo kwa  kutofanikiwa kupata ushindi katika uchaguzi.

Mapema mwaka huu hata hivyo aliweka wazi kwamba alichukua mapumziko kutoka kwa umma ili kuangazia muziki wake.

"Nilikuwa nimejifungia  tu kwenye Studio ya Nyumbani nikitengeneza Sauti Bora za Muziki kwa ajili yenu mashabiki wangu tangu siku ya kwanza," Bahati alisema kupitia ukuraa wake wa mtandao wa Instagram.

Alibainisha ilikuwa ni mapumziko ya mitandao ya kijamii ya kwanza aliyokuwa akichukua katika kipindi cha miaka kumi