"Mapenzi ya mitandaoni ni bandia!" Bahati alalamika baada ya Diana kukataa kumbusu siku tano

Mwimbaji huyo alieleza wasiwasi kuhusu mapenzi ya Diana Marua kwake.

Muhtasari

•Bahati aliibua wasiwasi kwamba madai kuwa Diana Marua hatimaye atamwacha siku moja huenda yakawa kweli

•Bahati alifichua kuwa mpenzi huyo wake amekuwa akikataa kumbusu siku kadhaa zilizopita tangu apate kidonda.

Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Siku ya Jumapili, wanandoa maarufu Kelvin 'Bahati' Kioko na Diana Marua walichapisha video kadhaa wakiwafahamisha mashabiki wao kuhusu maendeleo mapya zaidi katika maisha yao kama ilivyo kawaida yao.

Katika video hiyo, walizungumzia  jinsi walivyochoka baada ya kutumia muda wao kumhudumia binti yao mgonjwa.

Diana pia alifichua alikuwa ametumia muda mwingi na mwimbaji huyo wakizungumza  kuhusu masuala ya mapenzi.

"Namuuliza kipimo cha mapenzi ni kipi maana ako zile za  'Mpenzi, je unanipenda?," Diana alisema.

Wawili hao walionekana kuchoka sana na kuboeka.

Bahati aliibua wasiwasi kwamba madai ya mitandaoni kuwa mama huyo wa watoto watatu hatimaye atamwacha siku moja huenda yakawa kweli. Alikiri kwamba alikuwa na huzuni kwa sababu aliogopa kuachwa.

Ili kuthibitisha wasiwasi wake kuwa sio kweli, mwimbaji huyo alimthubutu Diana Marua kubusu mdomo wenye kidonda. Diana alimuuliza mumewe alipata wapi kile kidonda, akasogea kana kwamba anambusu lakini akaacha.

"Nijikute!" alisema.

Bahati alifichua kuwa mpenzi huyo wake amekuwa akikataa kumbusu siku kadhaa zilizopita tangu apate kidonda.

"Unataka kunikiss kwa camera na umekuwa ukikataa kunikiss siku tano ambazo zimepita kwa sababu ya kidonda. Mapenzi ya mitandao ya kijamii ni ghushi sana jameni," mwimbaji huyo wa zamani wa injili alisema.

Wawili hao waliendelea na mazungumzo yao huku wakifichua jinsi walivyo na mipango mikubwa kwa mashabiki wao mbeleni.

Katika video nyingine waliyochapisha mwezi jana, Diana alifichua jambo moja la kipekee ambalo anapenda kuhusu mumewe.

Mwanavlogu huyo alisema anapenda jinsi mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili huwa anapongeza urembo wake kikweli.

"Unajua ninachopenda kukuhusu? Unanipongeza kwa dhati," mwanavlogu huyo alimwambia mume wake.

Aliongeza, "Haijawahi kuwa uwongo.  Wakati mwingine ukikula huwa unanitazama tu na kuniambia, ',mpenzi wewe ni mzuri sana, mpenzi nakupenda. Asante kwa kuwa mke mzuri kwangu."

Bahati alisema kupongezana ni sehemu muhimu ya ndoa na akadokeza kuwa ndiyo siri ya muungano wenye mafanikio.

"Siri ya ndoa, Kupongezana!!" alisema.

Alikiri kuwa kwa kawaida yeye humpongeza Diana Marua na inasaidia kufanya ndoa yao kuwa imara zaidi.