WABUNGE KUUPITISHA MSWADA?

Nangoja kumuona mbunge atakayepiga kura kuupinga mswada wa fedha - rais Ruto

Rais amesema mzozo wa umma kuhusu Mswada wa Fedha wa 2023 sio wa kweli.

Muhtasari

• Kulingana na mtazamo wa Ruto, kila kiongozi anakubaliana na pendekezo la ushuru katika ujenzi wa nyumba.

• Haya yanajiri huku bajeti ya fedha 2023/2024 ikitarajiwa kufikishwa mbele wa Wabunge mnamo Juni 15.

ametetea mswada wa fedha wa 2023.
Rais Ruto ametetea mswada wa fedha wa 2023.
Image: Facebook

Rais William Ruto kwa mara nyingine amezungumza kuhusu mswada wa fedha 2023.

Rais amesema mzozo wa umma kuhusu Mswada wa Fedha wa 2023 sio wa kweli. 

Akizungumza Jumapili katika ibada ya kanisa, eneo la Leshuta kaunti ya Narok, Rais alisema kuwa viongozi wa muungano wa Azimio la Umoja wanaendeleza kuupinga mswada huo kwa sababu wako katika upande wa upinzani.

“Wacheni kuuweka mpango wa mchango wa nyumba katika siasa. Pia walio katika upinzani wanaupenda mpango huu, iwapo Azimio wangekuwa katika uongozi, wangesema kile ambacho nasema.”  Alisema.

Kulingana na mtazamo wa Ruto, kila kiongozi anakubaliana na pendekezo la ushuru katika ujenzi wa nyumba katika mswada wa fedha 2023 kwani ni mzuri kwa taifa.

“Itabidi tupitishe mswada huu ili Kenya iweze kunawiri. Kuna baadhi ya mapendekezo ambayo wabunge wanapaswa kupigia kura iwapo yatapelekwa kwenye bunge, binafsi, nangoja kumwona mbunge yeyote atakayeangusha mswada huu” alisema Rais.

“ Wale ambao wanatuambia mpango wa ujenzi wa nyumba usitishwe kidogo wanafaa kuambiwa ngoja ngoja huumiza matumbo.” Aliendelea.

Haya yanajiri huku bajeti ya fedha 2023/2024 ikitarajiwa kufikishwa mbele wa Wabunge mnamo Juni 15.

Kulingana na muungano wa Azimio la umoja, wamedokeza kuendeleza maandamano yao iwapo mswada huo hautakuwa umeangaziwa kwa matakwa yao, huku Naibu Rais Rigathi Gachagua akieleza kuwa mswada huo utapitishwa bungeni bila ya kubadilisha chochote. 

Haya yanajiri baada ya seneta ya Busia Okiya Omtatah kufika mahakamani wiki jana kuwasilisha ombi la kuupinga mswada huo, akiwatia moyo wabunge kwamba wasitishwe na yeyote huku, akieleza kwamba Rais hapaswi kuhusishwa na bunge katika kuupinga wala kuukubali mswada.

“Wabunge hawakuchaguliwa na rais, walichaguliwa na raia  ambao ndio wanalipa ushuru. Mkiangazia chochote katika bunge mnapaswa kutilia maanani matakwa ya raia waliowachangua.” Alisema Omtatah katika mtandao wake wa Twitter.