Fahamu kwa nini Karen Nyamu anataka kuongoza wanawake kuandamana uchi jijini Nairobi

Seneta Nyamu ametishia kuchukua hatua zisizo za kawaida iwapo maslahi ya kaunti ya Nairobi hayatazingatiwa bunge na seneti.

Muhtasari

•Karen Nyamu alisema kuwa yeye na wanawake wengine watavua nguo na kuandamana mjini iwapo kilio chao hakitasikilizwa.

•Karen alitaka vitongoji duni vya Nairobi vitambuliwe kama maeneo yaliyotengwa na kufaidika na fedha zinazotengewa maeneo hayo.

Karen Nyamu
Karen Nyamu
Image: HISANI

Seneta wa kuteuliwa Karen Njeri Nyamu ametishia kuongoza wakazi wa Nairobi katika kuchukua hatua zisizo za kawaida iwapo maslahi ya kaunti ya Nairobi hayatazingatiwa na bunge na seneti.

Wakati akitetea vitongoji duni vya Nairobi katika seneti, seneta huyo wa UDA alisema kuwa yeye na wanawake kutoka mitaa mbalimbali ya mabanda katika mji mkuu wa nchii watavua nguo na kuandamana mjini iwapo kilio chao hakitasikilizwa.

"Mazungumzo yametosha, tutajitafutia suluhu sisi wenyewe. Kama vile gavana Wavinya alisema kuwa Wakamba wana njia zao za kutatua mambo, Nairobi tutatafuta njia ya kutatua mambo yetu na kuwafanya wakaazi wetu wa vitongoji duni watambuliwe,” seneta Karen Nyamu alisema kwenye hotuba yake ya hivi majuzi katika seneti.

Karen alibainisha kuwa licha ya Nairobi kuwa mji mkuu wa nchi na kuwa na mitaa ya kifahari, kaunti hiyo pia ina maeneo mengine mengi ya viwango vya chini.

Alibainisha kuwa kilio cha wakazi wa mitaa ya mabanda ya Nairobi hakijasikika na hivyo kumchochea kuwaongoza wanawake kuandamana uchi ili wasikilizwe.

"Tumekuwa tukilia kama Nairobi kwa wakazi hawa wa makazi duni na tumepuuzwa kwa miaka mingi. Tutageukia njia zisizo za kawaida. Kama wanawake wa Nairobi, na wanawake wa Laini Saba na Kiboro na Mji wa Huruma,  tutavua nguo katika mji huu madam spika ili tupate umakini wa watunga sera katika nyumba hii (seneti) na wabunge kwa sababu Nairobi sio kaunti tajiri," alisema Karen.

Seneta huyo wa kuteuliwa wa UDA alibainisha kuwa kaunti ya Nairobi ndiyo makazi ya vitongoji duni kadhaa ambavyo wakaazi wake wanahitaji kuangaliwa vyema.

"Hali ya kusikitisha ambayo raia hawa wa Kenya wamekuwa wakiishi imeendelea kupuuzwa na watunga sera hawa na pia wabunge katika nyumba hii na zingine," alisema.

Karen alitaka vitongoji duni vya Nairobi vitambuliwe kama maeneo yaliyotengwa na kufaidika na fedha zinazotengewa maeneo hayo.