Kalonzo avunja kimya baada ya kinara wake Raila Odinga kuwepo katika dhifa ya Ikulu

Kalonzo alisema kwamba dhifa hiyo iliyowakutanisha Raila na Ruto katika ikulu haifai kuangaliwa zaidi ya kwamba ni kwa sababu ya ziara ya mfalme wa Uingereza.

Muhtasari

• Kalonzo pia alizungumzia mzaha ambao naibu rais Rigathi Gachagua alimtania wakati alihudhuria dhifa ya ikuluni kuhusu kongamano la hali ya hewa.

KALONZO MUSYOKA
Image: HISANI

Kinara mwenza katika muungano wa Azimio One Kenya, Kalonzo Musyoka ametoa tamko lake baada ya kinara mkuu Raila Odinga kuhudhuria dhifa ya kumkaribisha mfalme wa Uingereza, Charles III katika ikulu ya Nairobi jioni ya Jumanne.

Wengi walitamani kujua msimamo wa Kalonzo kuhusu Odinga kuwepo katika dhifa hiyo licha ya kwamba mrengo huo wa upinzani umekuwa ukiwapiga vita viongozi wanachama wake wanaofanay ziara katika ikulu kukutana na Ruto.

Akitoa tamko lake, Kalonzo ambaye kwa sasa amejukumiwa kuongoza maslahi ya upinzani katika kamati ya mazungumzo ya kitaifa pamoja na mwenzake kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah anayewakilisha serikali, alisema kwamba Odinga kuonekana katika ikulu wala si dalili yoyote ya kutoa mwelekeo wa kisiasa humu nchini.

Kalonzo pia alizungumzia mzaha ambao naibu rais Rigathi Gachagua alimtania wakati alihudhuria dhifa ya ikuluni wakati wa kongamano la hali ya hewa lililofanyika Nairobi wiki chache zilizopita.

“Unajua wakati mmoja wakati nilienda ikulu, DP alisema nilienda pale wakati wa kongamano la hali ya hewa, alifanya utani mkubwa na alisema kwamba eti nilifurahia chakula na mengine, sawasawa katika kiwango cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, ninaweza nikakwambia kwamba badhi yetu tuko kwenye orodha inayotusubiri ya kualikwa katika ziara ya kitaifa ya mgeni mkuu mwenye haiba kama ya mfalme Charles III, kwa hiyo haifai kuonekana zaidi ya hapo,” alisema.

Jioni ya Jumanne, Odinga alikuwa miongoni mwa wageni wachache walioalikwa katika ikulu ya Nairobi kweney dhifa ya kumkaribisha Malkia Camilla na mumewe Mfalme Charles.

Hii ni ziara ya kwanza kabisa katika taifa la umoja wa jumuiya ya madola kwa mfalme huyo ikiwa ni mwaka mmoja tangu alipotawazwa kama Mfalme kufuatia kifo cha mamake, malkia Elizabeth II.