Kisii: Polisi wanamtafuta mama aliyemlisha mwanawe kinyesi kwa kupoteza sindano

Chanzo kilisema kwamba mtoto huyo mdogo alikuwa akicheza na sindano hiyo ilipopotea na mamake akamhukumu kwa adhabu hiyo ya kinyama.

Muhtasari

• Baada ya tukio hilo kuzua hasira miongoni mwa majirani, mwanamke huyo alitoroka.

Picha ya maktaba ya gari la Polisi la Kitengela katika eneo la uhalifu hapo awali.
Image: MAKTABA

Polisi katika kaunti ya Kisii, eneobunge la Mugirango Kusini wanamsaka mama mmoja anayetuhumiwa kwa kumlisha mwanawe kinyesi cha binadamu kutoka chooni.

Kwa mujibu ya taarifa kutoka kituo kimoja cha habari kaunti ya Kisii, mama huyo ambaye hakuweza kutambuliwa kwa jina mara moja alimfanyia mwanawe kitendo hicho cha kinyama kama adhabu baada ya mtoto huyo kupoteza sindano ya kushonea nguo.

Chanzo kilisema kwamba mtoto huyo mdogo alikuwa akicheza na sindano hiyo ilipopotea na mamake akamhukumu kwa adhabu hiyo ya kinyama – kumlazimisha kula kinyesi alichokichota kutoka chooni.

Baada ya tukio hilo kuzua hasira miongoni mwa majirani, mwanamke huyo kutoka kijiji cha Bogetenga katka eneobunge hilo linaloongozwa na kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa, Silvanus Osoro, alichimba mitini.

Mpaka wakati taarifa hii ilipokuwa inaenda hewani, mwanamke huyo mwenye umri wa makamo alikuwa bado hajapatikana na polisi wamezidisha msako dhidi yake ili kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kunyanyasa mtoto kikatili.