Raila afichua mpango wa Ruto kumteua Chebukati kama Jaji Mkuu kabla ya uchaguzi 2027

Odinga alisema moja ya njia hizo Ruto amepanga kumteua aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka, IEBC Wafula Chebukati kama jaji mkuu.

Muhtasari

• Kiongozi huyo wa ODM alisema kulingana na njama hiyo, Jaji Mkuu Martha Koome atafaidika na Idara ya Mahakama kupata ufadhili wa ziada.

RAILA ODINGA
RAILA ODINGA
Image: SHABAN OMAR//THE STAR

Kinara wa upinzani Raila Odinga ameibuka na ufichuzi mpya wenye ukakasi akidai kwamba tayari rais William Ruto ameanza kuratibu njia za kujihakikisha ushindi katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Katika taarifa kwa vyombo vya umma Ijumaa Februari 2, Odinga alisema kwamba ana habari tendeti kutoka ndani ya bunge, ikulu na hata idara ya mahakama kwamba moja ya njia hizo Ruto amepanga kumteua aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka, IEBC Wafula Chebukati kama jaji mkuu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Kinara huyo wa ODM alipuuzilia mbali mambo ambayo serikali ilisema ilijadili na idara za mahakama na bunge katika mkutano wao wa ikulu wiki chache zilizopita.

Odinga alisema kwamba licha ya serikali kusema mkutano huo wa ikulu ulikuwa unahusu jinsi ya kuhakikisha uhusiano mwema baina ya taasisi huru, lakini ajenda kuu ilikuwa kuhusu jinsi yeye [Ruto] atashinda uchaguzi wa 2027.

“Katika makubaliano hayo, majaji watano wa mahakama ya juu na majaji wawili wa Mahakama ya Rufaa watakuwa wa Ruto kuwasilisha kwa JSC, na aliyataja majina, waliokuwa wenyeviti wa IEBC Wafula Chebukati na aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Ahmed Issack Hassan watateuliwa kuwa majaji wa Rufaa huku Chebukati baadaye akiinuliwa kama Jaji Mkuu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027,” Odinga alisema bila kutetereka.

Kiongozi huyo wa ODM alisema kulingana na njama hiyo, Jaji Mkuu Martha Koome atafaidika na Idara ya Mahakama kupata ufadhili wa ziada. Raila alithibitisha kuwa Koome tayari ametangaza kugombea nyadhifa hizo 11 katika notisi ya gazeti la serikali mnamo Ijumaa, Februari 2.

“Katika kikao hicho, Jaji Mkuu na Bw Ruto walifikia makubaliano ambayo yangemruhusu Bw Ruto kufadhili idara ya mahakama. Jaji Koome alikuwa atangaze nafasi za kazi za majaji watano wa ziada na majaji 11 wa Mahakama ya Rufaa. Tangazo la majaji hao 11 limetolewa leo. Liko kwenye gazeti la serikali la leo," Raila alisema.