Kijana wa miaka 28 anayeugua Seli Mundu aomba madaktari kumsaidia kufa

“Nimekuwa nikijua uchungu kama rafiki wa kawaida anayenijia kwa kushtukiza kuvuruga maisha yangu. Licha ya kuzoea hili, sikujua kwamba uchungu huu unazidi kuongezeka kadri umri unavyokwenda."

Muhtasari

• Baada ya kuona uchungu ukizidi kumtekenya ndani kwa ndani kwa mwendo wa aste, kijana huyo alisema kwamba aliamua kwenda mitandaoni kutafuta maelezo kuhusu ‘mtu kusaidiwa kufa’ .

Joe Mudukiza, mwathirika wa seli mundu
Joe Mudukiza, mwathirika wa seli mundu
Image: Facebok//Mudukiza Joe

Joe Mudukiza, kijana mwenye umri wa miaka 28 ametoa simulizi ya kudondosha machozi akielezea jinsi ambavyo amekuwa akipambana na ugonjwa wa seli mundu kwa maisha yake yote.

Akizungumza na jarida la Nation, Mudukiza alisema kwamba amefikia mahali katika maisha yake anaomba msaada kutoka kwa madaktari kumsaidia kukatisha maisha yake, ombi ambalo hata hivyo limeanguka katika masikio yaliyotiwa nta.

Mudukiza aliambia jarida hilo kwamba katika kipindi cha miezi 5 iliyopita, akili zake zimekuwa zikitawaliwa na wazo la kifo chake, lakini kwa nje amekuwa akiigiza kwamba yuko sawa huku ndani akiumia kwa uchungu.

“Kwa miezi mitano iliyopita, akili zangu zimekuwa zikifurikwa na wazo la kifo changu. Nimejaribu kuivaa barakoa ya ujasiri ambayo kila mtu wa karibu name anaizoea lakini ukweli ni kwamba ndani uchungu umeirarua barakoa hiyo,” alinukuliwa na Nation.

Kijana huyo alisema kwamba tangu agundulike kuwa na ugonjwa huo wa ukame wa damu mwilini, hajawahic furahia maisha yasiyo na uchungu mwilini na kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 26 iliyopita, ameamua kuonesha udhaifu wake hadharani.

“Nimekuwa nikijua uchungu kama rafiki wa kawaida anayenijia kwa kushtukiza kuvuruga maisha yangu. Licha ya kuzoea hili, sikujua kwamba uchungu huu unazidi kuongezeka kadri umri unavyokwenda. Tangu Aprili mwaka jana, maisha yangu yamechukua mkondo tofauti kabisa na hata uchungu ambao nimekwishauzoea umekuwa wa kunitisha kila siku,” alizidi kusimulia kwa uchungu.

Baada ya kuona uchungu ukizidi kumtekenya ndani kwa ndani kwa mwendo wa aste, kijana huyo alisema kwamba aliamua kwenda mitandaoni kutafuta maelezo kuhusu ‘mtu kusaidiwa kufa’ – jambo ambalo hata hivyo aligundua kwamba halijawahi tekelezwa nchini Kenya.

Baada ya kutafuta kwa muda, alipata huduma hizo zinatolewa nchini Ubelgiji na kuwaomba kumpa msaada huo lakini kizingiti kikubwa ni kwamba hakuna mtu wa karibu naye anaunga mkono hatua hiyo.

“Madaktari wangu wote wa humu nchini ambao wanastahili kutia saini katika mchakato wangu wa kwenda kusaidiwa kufa Ubelgiji wamekataa kuwa miongoni mwa watu wa kuchangia safari yangu kuelekea kaburini. Waliniambia kwamba wako katika taaluma ya kuokoa maisha, na si kuyamaliza,” aliongeza.

Kijana huyo alisema kwamba hakuwahi mshirikisha mtu yeyote wa familia na mama yake aligundua hili baada ya kuambiwa kwamba Mudukiza alichapisha kuhusu azma yake ya kusaidiwa kufa nchini Ubelgiji, jambo alilolisimulia kuwa lilimuumiza sana mamake.

Joe Mudukiza, mwathirika wa seli mundu
Joe Mudukiza, mwathirika wa seli mundu
Image: Facebok//Mudukiza Joe
Joe Mudukiza, mwathirika wa seli mundu
Joe Mudukiza, mwathirika wa seli mundu
Image: Facebok//Mudukiza Joe
Joe Mudukiza, mwathirika wa seli mundu
Joe Mudukiza, mwathirika wa seli mundu
Image: Facebok//Mudukiza Joe