Mike Sonko atoa gari lake kusimamia dhamana ya Ksh 700k ya Ian Njoroge

Sonko aliwakabidhi hadi stakabadhi 3 za umiliki wa magari yake na kuwaambia wachague gari moja lenye litawafaa katika kusimamia dhamana hiyo ya 700k kwa ajili ya Ian Njoroge lakini akaomba mamake ahakikishe asitoroke.

Muhtasari

• Kijana huyo wa miaka 19 ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu alinaswa kwenye kamera akimshambulia afisa wa polisi wa trafiki.

Image: x

Aliyekuwa gavana wa Nairobi na mjasiriamali Mike Sonko amejitolea kumdhamini Ian Njoroge, mshukiwa aliyenaswa kwenye kamera akimshambulia afisa wa poisi wa trafiki barabarani katika mtaa wa Kasarani wiki moja iliyopita.

Njoroge ambaye alifikishwa mahakamani Ijumaa aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki 7 ambazo familia yake ilishindwa kupata kumpelekea Mike Sonko kuingilia kati.

Katika video ambazo Sonko alipakia kwenye ukurasa wake wa X akiwa na Njoroge pamoja na wanafamilia wake, alionekana akiwakabidhi stakabadhi za umiliki wa magari.

Sonko aliwakabidhi hadi stakabadhi 3 za umiliki wa magari yake na kuwaambia wachague gari moja lenye litawafaa katika kusimamia dhamana hiyo ya 700k kwa ajili ya Ian Njoroge lakini akaomba mamake ahakikishe asitoroke.

“Kwa hiyo mtachagua gari moja kati ya haya matatu. Chagua moja lenye wakili ataona kama linafaa na linaweza kusimamia dhamana ya Ian Njoroge, lakini hakikisha bora asitoroke,” Sonko alisikika akiomba.

Katika uamuzi wa mahakama mnamo Ijumaa, hakimu mkuu mkaazi Ben Ekhumu alimuondolewa Ian Njoroge shtaka la wizi wa kimabavu na kusalia na mashtaka mawili ya kumshambulia afisa wa polisi na kukataa kutiwa mbaroni.

Jaji huyo alipinga ombi la mashtaka lililolenga kumzuia Ian Njoroge kutoachiliwa kwa dhamana.

Kijana huyo wa miaka 19 ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu alinaswa kwenye kamera akimshambulia afisa wa polisi wa trafiki kwa ngumi na mateke katika barabara ya Mirema huko Kasarani.