Mamake Ian Njoroge aomba radhi katika madai ya mwanawe kumshambulia polisi

Mamake Ian alikiri makosa yaliyofanywa na mwanawe kwa kumshambulia afisa wa polisi na makosa la trafiki.

Muhtasari

• Alipokamatwa mshukiwa alidai kwamba mlalamishi (polisi wa trafiki) alikuwa ametaka hongo kutoka kwake. 

• Ian Njoroge alikamatwa na kufikishwa mahakamani siku ya Jumanne na kukanusha mashtata yote dhidi yake.

Image: DOUGLAS OKIDDY

Mamake Ian Njoroge ameomba radhi kwa niaba ya mawanawe anayedaiwa kumshambulia afisa wa polisi.

Ruth Nyambura Mbagara, mama wa mvulana mwenye umri wa miaka 19 aliyenaswa kwenye video akimshambulia afisa wa polisi wa trafiki, amesema mwanawe kawaida ni mtu mwenye heshima na alishtuka kuona video ya mwanawe akimshambulia afisa wa polisi.

Mama huyo ambaye ni mfanyibiashara hata hivyo alimtetea mwanawe akisema kwamba huenda mvulana huyo alifanyiwa kitendo na afisa mlalamishi na kumkasirisha.

Huku akikiri kuwa Njoroge aligeuza gari kinyume na kanuni za trafiki mama huyo alidai kuwa afisa aliyemkamata aliitisha hongo ya Ksh.10,000 pesa ambazo mvulana huyo hakuwa nazo.

Madai ya kuitisha hongo pia yalitolewa na mshukiwa ambaye wakati akihojiwa punde tu baada ya kukamatwa alisema kwamba walikosana na polisi huyo kutokana na kiasi cha hongo alichokuwa akiitisha.

Kulingana na mamake, Ian alisema angeweza kuchangisha tu Ksh.5,000 kutoka kwa marafiki lakini afisa huyo alisisitiza kwamba angemuachilia tu akiwa angetoa elfu 10 hali iliyopelekea purukushani kati ya wawili hao.

Mamake Ian alikiri makosa yaliyofanywa na mwanawe kwa kumshambulia afisa wa polisi lakini alishikilia kwamba tukio hilo huenda lilichochewa pia na afisa huyo.

Mama huyo alisema siku hiyo mwanawe alikuwa kwa haraka kwenda kuchukuwa ndugu zake ili awapeleke kanisani kama ilivyokuwa desturi yake.

Ian alifikishwa mahakamani siku ya Jumanne na kufunguliwa mashtaka kadhaa yakiwemo wizi wa mabavu, kukataa kutiwa mbaroni, makosa ya trafiki na kumshambulia afisa wa polisi. Alikanusha mashata yote.