Hafla ya mchango wa kanisa aliyoalikwa Rachel Ruto yasitishwa baada ya Gen Z kutuma onyo kali

Usitisho huu unakuja kipindi ambapo vijana wameamua kuchukua katika mitandao ya kijamii kutangaza oparesheni ya kuhakikisha hakuna kufanyika kwa siasa kwenye mimbari na madhabahu.

Muhtasari

• Huku kukiwa na hasira ya umma kutokana na kuhudhuria kwa Bi Ruto, Kanisa la Lavington United Church lilitangaza kughairi ufadhili huo.

RACHEL RUTO
RACHEL RUTO
Image: FACEBOOK

Kanisa la Lavington United jijini Nairobi limelazimika kukubali shinikizo la vijana wa Gen Z mitandaoni na kusitisha hafla ya mchango wa kujenga kanisa ambayo mgeni wa heshima alikuwa ni mama taifa, Rachel Ruto.

Usitisho huu unakuja kipindi ambapo vijana wameamua kuchukua katika mitandao ya kijamii kutangaza oparesheni ya kuhakikisha hakuna kufanyika kwa siasa kwenye mimbari na madhabahu.

Shinikizo lilianza baada ya barua ya mwaliko kwa mchango huo uliotarajiwa kufanyika Jumapili kwa ajili ya ujenzi wa kanisa kuenezwa katika mitandao ya kijamii na watu walipoona Mke wa rais ndiye mgeni mwalikwa, walituma jumbe za onyo wakitahadharisha uongozi wa kanisa dhidi ya hatua hiyo.

Kadi ya mwaliko iliyotiwa saini na Mchungaji Simon Muhati inasomeka: “Timu ya Kichungaji na Uongozi wa Kanisa kwa moyo mkunjufu wanaalika…kwenye hafla ya kuchangisha pesa ili kukamilisha Patakatifu petu tarehe 30 Juni 2024 kuanzia saa 10 asubuhi katika Kanisa la Lavington United Church. Mgeni Mkuu atakuwa Mheshimiwa Rachael Ruto, EGH, Mke wa Rais wa Jamhuri ya Kenya.”

Kuonekana kwa kadi ya mwaliko wa kuchangisha pesa kwenye mtandao kuliwakasirisha Wakenya wengi, ambao walikashifu kanisa kwa kumwalika Bi Ruto na kutishia kuvamia harambee hiyo mnamo Juni 30.

Mwabili Mwagodi, ambaye alijitambulisha kama mshauri wa usimamizi wa uhasama kwenye X, alituma ujumbe mfupi kwa Mchungaji Mutahi: “Habari za jioni, Mchungaji Mutahi. Nilianza kampeni ya kuwaondoa wanasiasa kwenye mimbari ya kanisa nchini Kenya. Ninaona hapa kwamba umemwalika Bi Rachel Ruto kwenye kanisa lako kwa ajili ya kuchangisha pesa. Ujumbe huu ni wa kukuarifu kuwa tunakuja kwa uchangishaji. Mungu akubariki."

@SokoAnalyst, mtumiaji wa X, pia alishiriki kadi ya mwaliko, akisema “Ndugu Lavington United Church, tafadhali msiwajali wachinjaji watoto na walaghai. Mkiruhusu hili, basi mtakuwa washiriki pia. Huu upuuzi wa kuwapa wanasiasa na wenzi wao usikivu kanisani lazima ukome SASA.”

Huku kukiwa na hasira ya umma kutokana na kuhudhuria kwa Bi Ruto, Kanisa la Lavington United Church lilitangaza kughairi ufadhili huo.

"Timu ya Uongozi na Kichungaji ya Kanisa la Lavington United inapenda kuwajulisha washiriki kwamba Tukio la Kuchangisha Pesa lililopangwa kufanyika tarehe 30 Juni 2024 limeghairiwa," kanisa hilo lilitangaza Ijumaa.

Kenya imekuwa na msukosuko katika wiki iliyopita huku vijana wakiingia mitaani kupinga Mswada tata wa Fedha, unaopandisha ushuru wa bidhaa.