Morara Kebaso apendekeza jina la chama anachotaka kusajili

Amesema atatumia shilingi zilizosalia takribani laki moja kusajili chama hicho cha kisiasa

Muhtasari

• Morara amekuwa mkosoaji mkuu wa miradi ya serikali katika utawala wa Rais Dkt,. William Ruto.

• Tayari amebuni rangi za chama kuwa kijani kibichi na jina la chama kitakachosajiliwa ni INJECT Party 

Morara Kebaso
Image: HISANI

Wakili Morara Kebaso ambaye pia ni mfanyabiashara amedokeza kuwa anapanga kusajili chama cha kisiasa kutumia hela zilizobaki baada ya kununua seti ya viti.

Kupitia akaunti yake ya mtandao wa X, Kebaso amesema kuwa atalipa shilingi laki moja kusajili chama.

Wakili huyo anatarajiwa kuwasilisha stakadhi ikiwemo nakala mbili za katiba ya chama kwa ofisi ya msajili wa vyama vya kisiasa.

Morara ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa miradi ya serikali ya rais William Ruto,  amekitaka kizazi cha Gen Z kupanga na kuunda muungano wenye viongozi.

Awali katika maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024/25, waandamanaji wa gen z walikiri kukosa kiongozi maalum na maandamano yaliandaliwa kupitia mitandao ya kijamii.

Taarifa ya Morara inajiri siku moja baada ya ugomvi mkali kujitokeza mtandaoni haswa mtandao wa X baina yake na mwanaharakati Mercy Tarus kuhusiana uvumbuzi wa kauli mbiu 'Kenya Ni Home'.

Morara hata hivyo amesema kupitia chapisho kwenye mtandao wa X kuwa tatizo la Jumatano kuhusu kauli mbiu ya 'Kenya Ni Home' limetatuliwa.

Kebaso Morara aliomba Wakenya kumchangia hela kwa minajili ya kununua mitambo ya kupaza sauti atakayotumia kwa kampeni.

Aidha Morara amesema kuwa chama anachotaka kusajili kitaitwa Injection of National Justice, Economic and Civic Transformation (INJECT).

Vile vile, amesema rangi za chama zitakuwa kijani kibichi kuashiria mwanzo mpya na rangi ya dhahabu kuashiria kesho ya mafanikio.