Kwa nini Muhoozi anataka wafanyikazi wa baba yake Museveni kufutwa kazi

Jenerali Muhoozi anataka wasimamizi wa akaunti za mitandao ya kijamii za babake kupigwa kalamu.

Muhtasari

•"Watu wanaosimamia akaunti za mitandao ya kijamii za baba yangu wafutwe kazi! Aina hii ya habari ni za siri!" Muhoozi alisema

•Museveni kupitia akaunti yake ya Twitter alifichua kuwa serikali ya Kongo iliipatia Uganda kibali cha kushambulia kambi ya magaidi wa ADF.

KWA HISANI
KWA HISANI
Image: Muhoozi Kainerugaba

Mwanawe rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba amewataka wasimamizi wa akaunti za mitandao ya kijamii za babake kufutwa kazi.

Hii ni baada ya akaunti ya  Twitter ya rais Museveni kutumika kufichua maelezo ya shambulio la Uganda dhidi ya Congo DRC, habari ambazo kulingana Muhoozi, ni za siri.

"Watu wanaosimamia akaunti za mitandao ya kijamii za baba yangu wafutwe kazi! Aina hii ya habari ni za siri!" Muhoozi alisema kupitia Twitter.

Mapema siku ya Jumapili, Museveni kupitia akaunti yake ya Twitter alifichua kuwa serikali ya Kongo iliipatia Uganda kibali cha kushambulia kambi ya magaidi wa ADF.

Kiongozi huyo wa Uganda alijivunia shambulio hilo na kujigamba kuwa jeshi lake lina uwezo mkubwa wa magaidi wa ADF mahali popote wanapojificha.

"Siku ya Ijumaa, maadui walipata malipo yao wanayostahili. Popote watakapokwenda, tutawafikia mradi tu Serikali ya Kongo itaturuhusu kuwashughulikia. Hongera UPDF na pongezi kwa Serikali ya DRC na Jeshi la Kongo," alisema.

Mwanzoni, kauli pinzani ya Muhoozi kuhusu chapisho la babake ilichukuliwa na baadhi ya wanamitandao kama dharau kwake, madai ambayo alijitokeza kupinga baadaye.

"Baba yangu, Mheshimiwa Rais Yoweri Museveni, ni nabii wa Mwenyezi Mungu! Namheshimu kupita kawaida!!!"alisema.