"Nafikiria kujiunga na Lenana au Alliance" Nuru Okanga ajibu kuhusu alama alizopata katika KCPE

Alifichua kuwa ana familia ambayo angependa kuiona wikendi hata anapoendelea na masomo yake ya shule ya upili.

Muhtasari

•Nuru Okanga amesema ameridhishwa na alama ambazo Wakenya na vyombo vya habari wanadai alipata.

•Alipoulizwa ni shule gani ya sekondari anayotaka kujiunga nayo,  alibainisha kuwa analenga shule ya Lenana au Alliance.

ndani ya studio za Radio Jambo.
Nuru Okanga ndani ya studio za Radio Jambo.
Image: RADIO JAMBO

Mfuasi sugu wa kinara wa ODM Raila Odinga, Bw Nuru Okanga amesema ameridhishwa na alama ambazo Wakenya na vyombo vya habari wanadai alipata.

Akizungumza katika mahojiano na Mpasho, mfuasi huyo wa chama cha  ODM ambaye ananuia kuwania kiti cha MCA katika uchaguzi mkuu ujao alitangaza kuwa hawezi kuongeza wala kupunguza alama ambazo imedaiwa alipata.

Okanga alivishutumu vyombo vya habari kwa kuonyesha alama walizoonyesha bila kumuuliza iwapo zinapaswa kuonyeshwa kwa umma au la.

“Nilienda nikafanya mtihani kabisa na nikapost. Kila mahali wakajua Okanga amekalia mtihani. Na nilijua siku kama ya leo ama ya jana, kuna vitu zinakuja. Nilikuwa natarajia matokeo na kutrend,” Okanga alisema kwenye mahojiano ya Ijumaa.

Aliongeza, “Sasa hata wameacha namba moja Kenya mzima. Wameacha ata mtihani wenyewe, ata saa hii ukiuliza mtoto ni nani waziri wa elimu hajui. Anajua tu Okanga. Mimi naambia watu wa media, nilifanya mtihani wangu nikaweka hadharani. Kwa hivyo, alama mliweka nimeridhika nayo. Siwezi punguza na siwezi kuongea.”

Okanga alifanya mtihani wa KCPE 2023 katika Shule ya Msingi ya Mumias Muslim iliyoko kaunti ya Kakamega na ni miongoni mwa watahiniwa zaidi ya milioni moja waliopokea matokeo yao Alhamisi.

Alipoulizwa ni shule gani ya sekondari anayotaka kujiunga nayo, mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 32 alibainisha kuwa analenga shule ya Lenana au Alliance.

“Niko tayari kujiunga na shule ya bweni. Lakini yule principal wa Alliance ama Lenana School atakuwa anahakikisha kila Ijumaa jioni ananipea nafasi niende nikae na familia nyumbani. Jumatatu asubuhi niripoti shule, nadhani itakuwa sawa,” alisema.

Alifichua kuwa ana familia ambayo angependa kuiona wikendi hata anapoendelea na masomo yake ya shule ya upili.

Okanga pia alifichua kuwa timu ya Muungano wa Azimio inayoongozwa na kinara wake Raila Odinga tayari imempongeza kwa kutowaangusha.

Hapo awali, shabiki huyo sugu wa Raila Odinga mwenye umri wa miaka 32 alifichua kwamba aliamua kurejea shuleni na kukalia mtihani wake wa KCPE kama mtahiniwa wa kibinafsi ili apate vyeti vya kumruhusu kuwania kiti cha MCA wadi ya Kholera, eneo la Matungu katika uchaguzi mkuu wa 2027.