Babu Owino kumfadhili Nuru Okanga masomo yake ya sekondari hadi amalize

Kando na Babu Owino, wanasiasa wengine ambao walimhongera Okanga kwa juhudi zake ni kiongozi wa DAP-K, Eugene Wamalwa.

Muhtasari

• Hata hivyo, haijabainika wazi ni alama ngapi juu ya 500 ambazo Nuru Okanga alipata lakini wengi wamejitoma katika mitandao ya kijamii kumhongera.

Nuru Okanga
Nuru Okanga
Image: Facebook

Mtetezi mkali wa sera za Raila Odinga, Nuru Okanga ambaye licha ya umri wake mkubwa alirudi shule na kukalia mitihani ya KCPE mapema mwezi huu, amepata ufadhili wa masomo ya elimu ya sekondari.

Akitangaza ufadhili huo, mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino alimhongera na kusema kwamba atasimamia masomo yake ya shule ya upili hadi amalize.

“Hongera Nuru Okanga kwa Kufaulu Mitihani ya KCPE kwa Rangi zinazoruka.Nitakupa ufadhili wa kuendeleza Elimu yako ya sekondari.Mwalimu wa Hisabati hapa ni Wapi?” aliandika kwenye Facebook yake Babu Owino.

Hata hivyo, haijabainika wazi ni alama ngapi juu ya 500 ambazo Nuru Okanga alipata lakini wengi wamejitoma katika mitandao ya kijamii kumhongera kwa ujasiri wa kurudi shuleni.

Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 32 alikuwa miongoni mwa watahiniwa zaidi ya milioni moja na laki nne walioandika mtihani wa mwaka huu wa Cheti cha Elimu ya Msingi (KCPE). Licha ya kazi yake iliyodaiwa kubaki kuwa kitendawili, wanasiasa wa Azimio walimpongeza.

Kando na Babu Owino, wanasiasa wengine ambao walimhongera Okanga kwa juhudi zake ni kiongozi wa DAP-K, Eugene Wamalwa.

Kama tu Babu Owino, Wamalwa hakufichua alama alizopata Okanga.

"Hongera rafiki yangu Nuru Okanga kwa kufaulu mtihani wako wa KCPE kwa kishindo! Tunajivunia wewe na watu wa magharibi, Kaunti ya Kakamega, Eneo bunge la Matungu, Wadi ya Kholera! Hadithi yako ni ya kutia moyo ya kutochelewa kuhalalisha ndoto zako. ," Wamalwa alisema.

Baadae, Okanga aliandaa tafrija ya kusherehekea matokeo yake mjini Eldoret ambapo hata hivyo hajaweka wazi alama alizozipata.