Viongozi wengi mliowachagua ni wajinga - Babu Owino awaambia Wakenya

Babu pia alimtaka rais Ruto kutohitilafiana na mikopo ya HELB.

Muhtasari

• Mbunge huyo alisema viongozi wengi huendesha siasa kwa misingi ya kikabila, jambo ambalo alilitaja kuwa la kipumbavu.

Babu Owino
Babu Owino
Image: Facebook

Mbunge wa Embakasi East Babu Owino amewasuta Wakenya na kuwaambia kuwa hawafai kulia kuhusu ugumu wa maisha na mfumuko wa uchumi kwani ni wao walichagua viongozi.

Owino kupitia ukurasa wake wa Facebook, alisema kuwa katika taifa hili, kwa muda mrefu siasa zimekuwa zikiendeshwa kwa njia ya kikabila, kitu ambacho alikitaja kuwa gumzo lisilo la maana kabisa mpaka karne hii.

Owino alisema kuwa Wakenya wengi wanaendeleza upuuzi wa kufanya siasa kwa misingi ya Kikabila na mwisho wa siku wanakuja kulia kuwa maisha yamekuwa magumu, huku akisema viongozi wengi ambao Wakenya hao hao walichagua ni viongozi wapumbavu.

“Ni upumbavu tupu kwa viongozi kuwa wakabila katika nchi hii. Mara sisi kama Waluhya, Mara sisi kama Wakikuyu, Mara sisi kama wajaluo, huu ni upuuzi. Viongozi wengi mliowachagua ni wajinga,” Babu Owino alisema.

Mbunge huyo pia aligusia suala la rais Ruto kutaka kutupiliwa mbali mikopo ya elimu ya juu HELB akimtaka rais kukoma kuingilia suala hilo kabisa kwani wanafunzi wengi wanaofaidika na kutegemea mikopo hiyo hutoka katika familia za kimaskini mno.

"Ruto maneno ya Chuo Kikuu HELB wachana nayo Kabisa.Wenzio wanatoka katika malezi ya pole sana na Elimu PEKEE itawaokoa na Kongwa la umaskini linaloning'inia shingoni mwao," Owino ambaye ni mtetezi mkali wa sera za Raila Odinga alisema.

Rais Ruto alikuwa amesema kuna mipango ya kutoa mikopo ya HELB kwa elimu ya juu na badala yake kuweka kamati ya kushughulikia elimu katika taasisi za juu.