Siku ya Ukimwi Duniani

Washikadau waongeza juhudi za kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi nchini

Wakati wa hafla hiyo serikali ya Kaunti ya Kajiado pia ilizindua mkakati wa kukabiliana na maradhi ya ukimwi

Muhtasari

 

  • Kaunti ya Kajiado ina kiwango cha maambukizi ya Ukimwi cha asilimia 3.4
  • Waziri Kagwe alipongeza shirika la Beyond Zero kwa  kuongeza uekezaji katika sekta ya afya nchini akisema shirika hilo limepiga jeki uimarishaji wa huduma za afya kote nchini.

 

 Na PSCU

Wakenya leo walijiunga na ulimwengu mzima kuadhimisha siku ya Ukimwi Duniani huku wito ukitolewa wa kuimarisha juhudi za kupunguza maambukizi ya maradhi hayo nchini.

Hafla hiyo ilifanyika katika Kaunti ya Kajiado ambako serikali ya kaunti hiyo ilizindua mpango wa kukomesha maambukizi ya ugonjwa huo na kaswende kutoka kwa mama hadi kwa mtoto kufikia mwaka wa 2024. 

Mpango huo unaofadhiliwa na shirika linaloongozwa na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta la Beyond Zero utasaidia Kaunti ya Kajiado kutafuta rasilimali na kutekeleza mipango ya kukomesha maradhi hayo mawili.

Kaunti ya Kajiado ina kiwango cha maambukizi ya Ukimwi cha asilimia 3.4 huku kukiwa na idadi kubwa ya wanawake ya aslimia 4.5 wanaougua ugonjwa huo ikilinganishwa na idadi ya wanaume ya asilimia 2.3 katika kaunti hiyo yenye zaidi ya watu 30,000 walioambukizwa maradhi hayo.

Katika ujumbe wake Mama wa Taifa Margaret Kenyatta aliwataka washika dau kuongeza juhudi za kukomesha maambukizi ya virusi vya Ukimwi nchini kwa kuekeza katika mipango itakayosaidia kuwalinda raia ambao wamo hatarini ya kuambukizwa ugonjwa huo.

“Kuna haja kubwa ya kuongeza ufahamu na rasilimali kuzuia na kutibu virusi vya Ukimwi hasa miongoni mwa vijana, na kufanya kazi zaidi kulinda watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi kutokana na unyanyapaa na ubaguzi.

“Napigia debe kikamilifu juhudi za kumaliza maambukizi mapya na kukabili maambukizi ya HIV na Ukimwi kutoka kwa mama hadi mtoto. Naendelea kuwahimiza akina mama kwenda kufanyiwa ukaguzi mara nne bila malipo kabla ya kujifungua,” kasema Mama wa Taifa.

 Katika taarifa yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mshirikishi wa Wizara Dkt Mercy Mwangangi, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema Kenya itakabili virusi vya HIV kupitia mbinu mbali mbali zinazojumuisha uhamasishaji, kuchukuliwa kwa hatua kabambe na kutoa rasilimali zinazohitajika.

 Waziri Kagwe alipongeza shirika la Beyond Zero kwa  kuongeza uekezaji katika sekta ya afya nchini akisema shirika hilo limepiga jeki uimarishaji wa huduma za afya kote nchini.

 “Juhudi za kila mara za Mama wa Taifa Margaret Kenyatta za kuunga mkono mpango wa serikali wa Linda Mama chini ya Mpango wa Afya Bora kwa Wote zimewafanya akina mama wengi kujifungulia katika hospitali wakisaidiwa na wataalamu,” kasema Waziri huyo wa Afya.

 Wakati wa hafla hiyo serikali ya Kaunti ya Kajiado pia ilizindua mkakati wa kukabiliana na maradhi ya ukimwi wa awamu ya pili, mpango wa Kaunti ya  Kajiado wa kupambana na Ukimwi na magonjwa ya zinaa wa awamu ya pili na pia mashine ya kisasa ya mtu binafsi kujifanyia uchunguzi wa virusi vya HIV na Ukimwi.