Uhusiano wa raia na Polisi

Rais Kenyatta atoa wito kwa Wakenya kuunga polisi mkono katika kudumisha sheria na utangamano

Maafisa wa polisi sio adui. Ni marafiki wetu.

Muhtasari
  • Dkt Fred Matiang'i, ambaye pia alizungumza kwenye sherehe hiyo ya kuanzisha ujenzi alimpongeza Rais Kenyatta kwa kuweka marekebisho mbalimbali ambayo yameimarisha utendaji kazi wa sekta ya usalama nchini.
  • Rais Kenyatta alisema hayo Jumanne alasiri huko Ngong, katika Kaunti ya Kajiado ambako aliongoza hafla ya kuzindua ujenzi wa Chuo cha Uongozi wa Huduma ya Polisi ya Kitaifa.
Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta Rais Uhuru Kenyatta
Image: MERCY MUMO

Rais Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa Wakenya kuunga mkono polisi na mashirika mengine ya usalama katika juhudi za kudumisha  sheria na utangamano akisema maafisa wa polisi wanatekeleza kazi kubwa kudumisha usalama nchini.

Wakati huo huo, Kiongozi wa Taifa alikariri kujitolea kwa serikali yake kuhakikisha Huduma ya Polisi ya Kitaifa imepewa rasilimali za kutosha ili kutekeleza majukumu yake kikamilifu na vyema.

“Maafisa wa polisi sio adui. Ni marafiki wetu. Ni jukumu letu kama raia kutii sheria na kufanya tunachaogizwa kufanya kuambatana na sheria. Iwapo tutaendelea hivyo, nina imani kwamba taifa letu litakuwa salama na lenye ufanisi,” kasema Rais.

Rais Kenyatta alisema hayo Jumanne alasiri huko Ngong, katika Kaunti ya Kajiado ambako aliongoza hafla ya kuzindua ujenzi wa Chuo cha Uongozi wa Huduma ya Polisi ya Kitaifa.

Ujenzi wa chuo hicho utachukua mwaka mmoja kwa gharama ya takriban shilingi Bilioni moja na unafadhiliwa na Benki Kuu nchini kama sehemu moja ya ushirikiano mrefu na mkubwa kati ya polisi na taasisi hiyo ya kifedha.

Chuo hicho cha kisasa, kitakachojengwa katika kipande cha ardhi ya umma ya ekari 18 katika mji mdogo wa Embulbul, kitajumuisha ujenzi wa nyumba 220, madarasa, ukumbi wa mikutano wenye uwezo wa kuketi watu 450, chumba cha kupikia na vile vile ukumbi wa mankuli na vifaa vya michezo.

Rais alisema kwamba ujenzi wa chuo hicho cha uongozi ni sehemu moja ya mabadiliko katika huduma ya polisi ili kuiwezesha kufanikisha utendakazi bora na kushughulikia kikamilifu mahitaji ya udumishaji sheria katika karne ya 21.

“Baada ya kuchukua hatamu za uongozi wa nchi yetu, serikali yangu ilianzisha mpango madhubuti wa marekebisho wa sekta ya usalama ulionuiwa kuiwezesha kuhudumia Wakenya vyema zaidi.

“Tangu wakati huo, tumeboresha maradufu ufadhili wa sekta ndogo ya polisi licha ya kuimarisha maslahi na uwezo wa sekta ya usalama,” kasema Rais.

Alielezea kununuliwa kwa zaidi ya magari 3000 ya polisi kwa mtindo wa kukodisha, ujenzi na kuweka vifaa mahabara ya kisasa ya uchunguzi na kuajiriwa maafisa zaidi kuwa baadhi ya mafaniikio yalioafikiwa katika juhudi za kurekebisha kikosi hicho cha kudumisha sheria.

Rais aliusifu ushirikiano kati ya Huduma ya Polisi nchini na Benki Kuu nchini katika kuanzisha chuo hicho akisema mpango huo ni mfano mwema wa jinsi mtindo wa ushirikiano wa Serikali Nzima unavyofanya kazi chini ya utawala wake.

“Hafla ya leo ni ushahidi wa hivi karibuni wa jinsi taasisi za serikali zinaweza kuungana pamoja na kushirikiana na kuimarisha utoaji wa huduma,” kasema Kiongozi wa Taifa.

Rais Kenyatta alisema kwamba serikali imetilia mkazo taratibu za kushirikisha mashirika mbalimbali katika usimamizi wa usalama kwa kuondoa vizuizi vya kimuundo ambavyo vimetatiza utoaji mwafaka wa huduma za usalama siku za mbeleni.

Hivi karibuni, nimezindua Idara ya Kitaifa ya Huduma za Ndege pamoja na Huduma ya Mawasiliano ya Simu ya Usalama wa Kitaifa ambayo ni mipango inayolenga kuwianisha na kuimarisha utendakazi wa shughuli za mashirika mbalimbali," kasema Rais.

Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang'i, ambaye pia alizungumza kwenye sherehe hiyo ya kuanzisha ujenzi alimpongeza Rais Kenyatta kwa kuweka marekebisho mbalimbali ambayo yameimarisha utendaji kazi wa sekta ya usalama nchini.

“Katika muda wa miaka mitatu iliyopita, Mheshimiwa umekuwa ukitekeleza ajenda ya mabadiliko kuhusu vipi polisi wanaenda kusimamiwa na kupewa vifaa ili kufanya kazi na kuleta matokeo bora,” kasema Dkt Matiangi.

Gavana wa Benki Kuu nchini Dkt Patrick Njoroge na Inspekta Jenerali wa Huduma ya Taifa ya Poilisi Hilary Mutyambai pia walizungumza kwenye sherehe hiyo ambayo ilihudhuriwa na Gavana wa Kaunti ya Kajiado Joseph Ole Lenku miongoni mwa viongozi wengine wa eneo hilo pamoja na maafisa wakuu serikalini.