Kasisi alimuua mama na mwanawe kabla ya kujiua

Charity Cheboi
Charity Cheboi
Image: HISANI

Kasisi mmoja wa kanisa Katoliki Kevin Kipkoech alimnyonga mama na mtoto wake wa kiume kabla ya kujitia kitanzi katika Nyumba za Serikali zilizoko Barabara ya Jogoo mjini Nairobi, polisi wamebaini.

Maafisa wanaochunguza mauaji hayo, ambayo yaligunduliwa Februari 23 wamebaini kuwa Kipkoech alimuua kwanza Charity Cheboi na mtoto wake Allan Kipngetich kwa kuwanyonga kabla ya kujiua saa kadhaa baadaye.

Maafisa wa ujasusi walizuru tena eneo la tukio siku ya Jumamosi Februari 27 kabla ya kufanya hitimisho kuhusu ripoti yao ya mwisho.

 

Maafisa hao walisema waligundua kwamba Kipkoech alikuwa amejifungia chooni kwa kufuli. Ni katika choo ambamo mwili wake ulipatikana.

“Kama kungekuwa na mtu mwingine ndani ya nyumba hakuna vile angeweza kufunga choo kutoka ndani. Inaonekana ni mtu aliyekufa aliyeifunga ili kuongeza dhamira yake kufa, ”alisema afisa mmoja aliyehusika katika uchunguzi huo.

Wapelelezi kutoka Kitengo cha jinai wanasema hawajabaini sababu ya mauaji hayo.

Wanapanga kutembelea Seminari ya St Thomas Aquinas huko Karen, Nairobi, ambapo Kipkoech alisoma na alikuwa katika mwaka wa nane akilenga kuhitimu kama kasisi wa Katoliki mwaka huu, kupata habari zaidi juu ya tabia yake.

Cheboi na Kipngetich wanatarajiwa kuzikwa Alhamisi katika kijiji chao huko Elgeyo Marakwet. Wanatoka kijiji kimoja na Kipkoech.

Uchunguzi uligundua kuwa Cheboi na Kipngetich walifariki kutokana na kukosa hewa. Hii hufanyika wakati mtu ameuawa kwa kufunika pua na mdomo.

Mwanapatholojia mkuu wa serikali Dkt Johansen Oduor alisema mkono au kitambaa kiliwekwa kinywani na puani mwa mama na mtoto ili kuwanyima oksijeni.