Uhuru kuhutubia taifa kuhusu mikakati ya kudhibiti Covid-19

Muhtasari

• Hotuba ya rais inajiri wakati taifa linashuhudia ongezeko katika maambukizi ya virusi vya corona.

• Rais Kenyatta anatarajiwa kulegeza au kukaza zaidi masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya covid-19.

Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta hivi leo anatarajiwa kutangaza mipango na mikakati mipya ya serikali kudhibiti maambukizi ya virusi vya COVID-19.

Hotuba ya rais inajiri wakati taifa linashuhudia ongezeko katika maambukizi ya virusi vya corona.

Wataalam wa maswala ya kiuchumi hata hivyo wamekuwa wakionya kuhusu kuzidishwa kwa muda wa kafyu na masharti makali ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya covid-19 kutokana na athari za mikakakati hiyo kwa mapato na hali ya kiuchumi ya wananchi.

 

Hotuba ya rais Kenyatta pia inajiri siku moja tu baada ya kinara wa upinzani Raila Odinga kufichua kwamba ameambukizwa virusi vya covid-19. Raila amekuwa katika Nairobi Hospital kuanzia siku ya Jumatano na anajendelea kupokea matibabu huku hali yake ikiwa thabiti.

Rais Kenyatta anatarajiwa kulegeza au kukaza zaidi masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya covid-19. Hotuba ya rais inajiri wakati taifa linakabiliana na wimbi la tatu la maambukizi ya COVID-19.

Siku ya Jumatano Kenya ilisajili kiwango cha maambukizi cha asilimia 14 huku jumla ya watu 713 wakithibitishwa kuambukizwa  kutoka kwa sampuli 5,239 chini ya saa 24 idadi ya juu zaidi ya maambukizi mwaka huu.

Ni takriban mwaka mmoja tangu serikali itangaze masharti makali ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona mwezi Machi mwaka uliyopita wakati taifa lilisajili kisa cha kwanza cha maambukizi.

Serikali imepiga hatua muhimu katika mikakati ya kudhibiti maambukizi ya COVID-19 kwa kuzindua zoezi la utaoji wa chanjo dhidi ya virusi hivyo huku takriban watu nusu milioni wakitarajiwa kupokea chanjo hiyo katika awamu ya kwanza.