Sonko ataka hakimu Douglas Ogoti kujiondoa katika kesi ya ufisadi dhidi yake

Muhtasari

• Anasema kwamba anahofia mwelekeo ambao kesi yake imechukuwa na anataka ihamishiwe katika mahakama kuu kutoka mahakama ya chini.

• Anataka pia korti isimamishe kesi hiyo katika korti ya hakimu wakisubiri uamuzi wa ombi lake.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko amemshutumu hakimu wa mahakama ya ufisadi Douglas Ogoti kwa upendeleo na anataka ajiondoe katika kesi ya jinai inyaomkabili.

Sonko siku ya Jumatatu alisema ikiwa Ogoti ataruhusiwa kuendelea kusikiliza kesi dhidi yake basi huenda akavuruga kesi yake na kumsababishia hasara ambayo haiwezi kurekebika.

Anasema kwamba anahofia mwelekeo ambao kesi yake imechukuwa na anataka ihamishiwe katika mahakama kuu kutoka mahakama ya chini.

"Haki haipaswi kufanywa tu lakini lazima ionekane kutendeka," alisema.

Aliambia mahakama kuwa aliwahi kumuuliza hakimu ajiondoe kwenye kesi yake.

Hata hivyo kabla ya ombi lake la kukataa jaji huyo kusikiza kesi yake wakili wake alijiondoa kwenye kesi hiyo.

"Mwombaji ana wasiwasi ya kutosha kwamba wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake mbele ya hakimu mkuu wa Douglas Ogoti, uakilishi bora, haki na kutopendelea havitakuwepo na haoni kama haki zake za msingi katika kesi hiyo zitazingatiwa, ”Alisema gavana huyo wa zamani.

Aliongeza: “Mungozo wa sheria ni nguzo kwa demokrasia yetu na unapaswa kulindwa, kukuzwa na kutetewa wakati wote. Kinachoendelea katika mahakama ya mshtakiwa wa tatu (Ogoti) ambapo mwombaji amenyimwa haki ya kusikilizwa ni ukiukwaji wa haki yake ya kimsingi. "

Sonko anataka kesi hiyo ipewe hakimu mwingine wa mamlaka kama hiyo na sio Ogoti ili kuhakikisha kuwa anapata haki katika kesi dhidi yake.

Anataka pia korti isimamishe kesi hiyo katika korti ya hakimu wakisubiri uamuzi wa ombi lake.

Mnamo Machi 4 hakimu Ogoti alitoa uamuzi kukataa kujiondoa katika kesi hiyo akisema hakuna ushahidi wa mapendeleo.

Ogoti alikuwa amesema Sonko lazima aonyeshe sababu za kibinafsi au sababu za kimahakama kwa yeye kujiondoa.

"Sioni uthibitisho wowote wa upendeleo. Maombi ya Sonko hayana msingi wowote na yametupiliwa mbali," alikuwa ameamua.

Sonko na washtakiwa wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya ufisadi mbele ya Ogoti. Walikuwa wamekanusha mashtaka.